1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikosi cha Afrika Mashariki chaanza kuondoka Kongo

3 Desemba 2023

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamearifu kuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imeamua kutorefusha muda wa kikosi cha kulinda amani cha kikanda.

https://p.dw.com/p/4Zixg
Kikosi cha kanda ya Afrika Mashariki, mashariki mwa Kongo.
Picha hiyo inawaonesha wanajeshi wa kikosi cha kikanda cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichotumwa Kongo kurejesha utulivu. Picha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Kikosi hicho kilitumwa nchini Kongo Novemba mwaka jana kujaribu kurejesha utulivu upande wa mashariki unaondamwa na ukosefu mkubwa wa usalama.

Kilipelekwa mahsusi kushughulikia wimbi jipya la mashambulizi la kundi la waasi wa M23.

Taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa na Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya mkutano wa wakuu wa nchi imesema Kongo imeamua kuterefusha muda wa kikosi hicho nchini humo baada ya Disemba 8, 2023.

Inaarifiwa tayari kikosi hicho kimeanza kuondoka nchini Kongo leo Jumapili.

Msemaji wa kikosi hicho nchini Kongo amearifu kuwa kundi la kwanza la kiasi wanajeshi 100 wa Kenya limeondoka mapema Jumapili asubuhi kutoka uwanja wa ndege wa mji wa Goma kuelekea Nairobi.

Shirika la habari la AFP limeripoti kuiona ndege iliyobeba wanajeshi hao ikiruka mnamo alfajiri.

Hakuna maelezo ya ziada kuhusu ratiba ya kuondoka kwa wanajeshi wengine wa kikosi hicho kinachojumuisha pia wanajeshi wa Uganda, Burundi na Sudan Kusini.

Kongo ilikituhumu kikosi hicho kutotimiza wajibu 

Hatma ya kikosi hicho ilikuwa mashakani tangu rais Felix Tshisekedi wa Kongo kukikosoa na serikali yake kusema kimeshindwa majukumu yake ipasavyo.

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Picha: Pool Vlad Vanderkelen/Belga/picture alliance

Duru zinasema kikosi kingine kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, kitapelekwa kuchukua nafasi ya kikosi cha Afrika Mashariki.

Hata hivyo hadi sasa hakuna tangazo lolote juu ya tarehe ya kuwasili kikosi hicho au ufafanuzi wa nguvu itakayokuwa nacho pindi kitakapowasili mashariki mwa Kongo.

Mabadiliko hayo yanaashiria jinsi ilivyo vigumu kurejesha utulivu kwenye majimbo ya mashariki mwa Kongo ya Kivu Kaskazini na Ituri, ambako serikali ya nchi hiyo iliyaweka chini ya utawala wa kijeshi kushughulikia ukosefu wa usalama.

Kuondoka kwa kikosi cha Afrika Mashariki kumetangazwa wakati waasi wa M23 wameendelea kufanya hujuma zao na kusogea karibu kabisa na mji mkubwa wa Goma.

Hali hiyo imeongeza wasiwasi zaidi wa kudodora kwa hali ya usalama hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani nchini Kongo unaotarajiwa mnamo Disemba 20.

Kwa miaka kadhaa sasa, makundi ya wabeba silaha yamelitumbukiza eneo la mashariki mwa Kongo lenye utajiri mkubwa wa madini kwenye hamkani isiyo mfano. Makundi hayo ni matokeo ya vita vilivyoshuhudiwa nchini humo kati ya miaka ya 1990 na 2000.

Je, MONUSCO kufuata nyayo za kikosi cha Afrika Mashiriki?

Waasi wa M23 wanaoongozwa na jamii ya Watutsi wamechukua udhibiti wa maeneo makubwa ya ardhi kwenye jimbo la Kivu Kaskazini tangu walipoingia tena msituni mwishoni mwa mwaka 2021 baada ya kusitisha vurugu zao kwa miaka kadhaa.

Kifaru cha kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo.
Kikosi cha MONUSCO kimekuwepo nchini Kongo tangu mwishoni mwa miaka ya 1990.Picha: Djaffar Sabiti/REUTERS

Umoja wa Mataifa unakadiria watu 450,000 wamelazimishwa kuyaacha makaazi yao katika muda wa wiki sita zilizopita kutokana na mapigano. Watu 200,000 kati yao hawana njia za kufikiwa na msaada wa kiutu.

Kwa jumla watu wasiopungua milioni 7 wameyahama maskazini zao nchini Kongo, na wengi ni kutoka upande wa mashariki.

Kikosi cha Afrika Mashariki kilikuwa sehemu ya juhudi za muda mrefu za kurejesha utulivu mashariki mwa Kongo.

Umoja wa Mataifa umekuwa na kikosi cha kulinda amani nchini Kongo, MONUSCO, tangu mwaka 1999.

Lakini chenyewe pia kinalaumiwa kwa kushindwa kutimiza majukumu yake na serikali mjini Kinshasa imetaka nacho kiondoke ifikapo Januari, 2024.