1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mrengo wa Jubilee unaompinga Kenyatta wajitenga na Azimio

Thelma Mwadzaya14 Juni 2023

Mpasuko katika chama cha upinzani cha Jubilee umechukua mkondo mpya baada ya kundi linaloongozwa na kaimu katibu mkuu Kanini Kega kutangaza azma ya kujitenga na muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja.

https://p.dw.com/p/4SYFQ
Kenia Nairobi | Jubilee Party hält National Delegates Council trotz interner Krise ab
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Mahasimu wao chamani wamepuuzilia mbali taarifa hizo na kushikilia kuwa Jubilee iko imara. Chama cha Jubilee cha rais mstaafu Uhuru Kenyatta kinaandamwa na mivutano ya uongozi huku upande unaomuunga mkono Kenyatta ukiishtumu serikali kuchochea mgogoro huo.

Kwenye notisi iliyowasilishwa na kaimu katibu mkuu ambaye pia ni mbunge wa jumuiya ya Afrika mashariki, EALA, Kanini Kega aliweka bayana kuwa uamuzi huo ulifikiwa kwenye kikao cha kamati kuu kilichofanyika tarehe 6 mwezi huu wa Juni.

Mara baada ya tangazo hilo, upande wa Jubilee unaoongozwa na Jeremiah Kioni ulipuuzilia mbali notisi hiyo ukiitaja kutokuwa na ukweli. Kupitia mtandao wa Twitter, upande huo wa Kioni uliwasilisha ujumbe kuwa chama cha Jubilee  ni mshirika wa kudumu wa muungano wa upinzani wa Azimio na kwamba waliochoka nao wajondoe kimyakimya. Naibu Mwenyekiti wa mrengo huo David Murathe anaunga mkono kauli hizo.

Soma pia: Mzozo wa kisiasa ndani ya chama cha upinzani cha Jubilee unazidi kutokota

Notisi hiyo ya kujiondoa inatolewa ikiwa imepita wiki moja tangu upande unaoongozwa na kaimu katibu mkuu Kanini Kega kutangaza kongamano kuu maalum la wajumbe lililopangwa kufanyika tarehe 22 mwezi wa Julai mwaka huu kwenye ukumbi wa kimataifa wa KICC.

Mvutano waendelea

Kenia Nairobi | Jubilee Party hält National Delegates Council trotz interner Krise ab
Rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta Picha: Shisia Wasilwa/DW

Itakumbukwa kuwa kongamano jengine la kitaifa la Jubilee lililoongozwa na rais mstaafu Uhuru Kenyatta lilifanyika mtaani Ngong Racecourse mwishoni mwa mwezi uliopita. Kwenye kikao hicho,mrengo unaoongozwa na Jeremiah Kioni ulitangaza mabadiliko ya uongozi kwenye baraza kuu.

Mbunge wa viti maalum Sabina Chege aliyekuwa naibu kiranja wa upinzani bungeni aliondolewa na nafasi yake kukabidhiwa mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje.

Soma pia: Kenyatta: Ruto anataka kukinyakua chama cha Jubilee

Hatua hiyo ilizusha sintofahamu na wiki iliyopita, wabunge wa upinzani walizua purukushani pale Spika wa taifa alipokataa katakata kumvua Sabina Chege kofia ya kiranja wa upinzani kwa madai kuwa mahakama imemfunga mikono.Moses Wetangula ni Spika wa bunge la taifa.

Kwa sasa kambi ya kaimu katibu mkuu Kanini Kega inadhamiria kuwaondoa viongozi waliounda chama cha Jubilee.Musalia Mudavadi ni Waziri Kiongozi nchini Kenya na huu ndio mtazamo wake. Mahasimu chamani Jubilee wanajiandaa kwa kongamano maalum ifikapo tarehe 22 mwezi wa Julai.