1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo ndani ya chama cha Jubilee unazidi kutokota

Saumu Njama Thelma Mwadzaya
23 Mei 2023

Mzozo wa kisiasa ndani ya chama cha upinzani cha Jubilee unazidi kutokota baada ya msajili wa vyama vya siasa kuidhinisha mchakato wa kusitisha uanachama wa viongozi wanaoegemea kambi ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

https://p.dw.com/p/4RiOB
Kenia Nairobi | Jubilee Party hält National Delegates Council trotz interner Krise ab
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Hata hivyo wanasiasa hao wamekwenda mahakamani na chombo hicho kimeamuru mipango ya kutimuliwa kwao isisimame kusubiri uamuzi kamili mwishoni mwa mwezi huu. 

Soma pia: Kenyatta: Ruto anataka kukinyakua chama cha Jubilee

Siku moja baada ya kambi ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta ya chama cha Jubilee kukutana na kuwatimua mbunge wa viti maalum Sabina Chege na mwenzake wa bunge la afrika mashariki, EALA,Kanini Kega, kwa tuhuma za uasi, msajili wa vyama vya siasa Anne Nderitu amethibitisha kuwa mchakato wa kuwaondoa viongozi wanaoegemea upande wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta ulifuata sheria. Msajili wa vyama vya siasa Anne Nderitu aliweka bayana kuwa chama kilifuata sheria kuwaondoa katibu mkuu Jeremiah Kioni na naibu mwenyekiti David Murathe.Uamuzi huo pia umethibitisha kuwa mweka hazina Kagwe Gichohi amesimamishwa uanachama wa Jubilee.Kanini Kega ni mbunge wa Jubilee wa Afrika mashariki, na mwanasiasa anayejitambulisha sasa kuwa kaimu katibu mkuu halali wa chama hicho.

 Soma pia: Upinzani wa Kenya waishutumu serikali kwa kuchochea matabaka

Hatma ya usimamizi wa kamati kuu ya chama

Kenia Nairobi | Jubilee Party hält National Delegates Council trotz interner Krise ab
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Itakumbukwa kuwa kambi hii ilimkabidhi mbunge wa viti maalum Sabina Chege nafasi ya kaimu kiongozi wa chama sintofahamu zilipoanza.Hatua hii inamuweka rais mstaafu Uhuru Kenyatta katika nafasi ngumu kwani hana usimamizi kamili wa kamati kuu ya chama cha Jubilee.Kadhalika Uhuru Kenyatta ni mwenyekiti wa baraza la chama cha Azimio la Umoja One Kenya kwani Jubilee ni moja ya vyama vya msingi. Kwenye kongamano kuu la wajumbe hapo siku ya Jumatatu, rais mstaafu alisisitiza kuwa Jubilee iko hai.

Ifahamike kuwa msajili wa vyama Anne Nderitu kadhalika amekifutilia mbali kikao cha kamati kuu kilichoitishwa na Uhuru Kenyatta kwa misingi kuwa idadi ya waliohudhuria haikutimiza vigezo.Kikao hicho kilifanyika tarehe 28 mwezi wa Aprili mwaka huu.

Yote hayo yakiendelea, wandani wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta sasa wanatishia kuandamana kwa kile wanachokitaja kuwa hujma kwa siasa za vyama vingi.Wakiongozwa na mbunge wa zamani wa Ndaragwa Jeremiah Kioni aliyezungumza na waandishi wa habari alisisitiza kuwa barua hiyo ya kuwatimua chamani ina mkono wa fitna na utundu kwani ilitakiwa kuwasilishwa kwa baraza kuu ndipo mchakato ukamilike.Martha Karua ni kiongozi wa NARC Kenya iliyo kiungo muhimu kwenye Azimio la Umoja One Kenya na anaamini kuwa wanaowavuruga sio waasi wa chama.

Wakati huohuo,wabunge wa muungano tawala wa Kenya Kwanza wamekutana ikulu ya Nairobi hii leo kwenye kikao cha sita cha aina hiyo kujadili ramani ya taifa.Ajenda kuu ni kuupitisha muswada wa fedha wa 2023 unaonuwia kuiongezea serikali kuu mapato kupitia kodi.