1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Afghanistan imeangushwa na makubaliano ya Doha

30 Septemba 2021

Jenerali Frank McKenzie wa wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon amesema kuporomoka kwa serikali ya Afghanistan mwezi Agosti huenda ikawa kumetokana na makubaliano ya mwaka 2020 kati ya Marekani na kundi la Taliban.

https://p.dw.com/p/41598
Kabul, Afghanistan | General Kenneth McKenzie
Picha: Sajjad Hussain/AFP/Getty Images

Jenerali Frank McKenzie, wa Kamanda Kuu ya Kijeshi, ameiambia Kamati ya Seneti kuhusu Masuala ya Kijeshi, kwamba mara tu idadi ya wanajeshi wa Kimarekani mjini Kabul ilipoanza kupungua chini ya 2,500 kutokana na amri ya Rais Joe Biden, ndipo serikali ya Afghanistan nayo ilipoanza kusambaratika.

Jenerali McKenzie ameongeza kwamba kusainiwa kwa makubaliano hayo ya Doha, mnamo Februari 29, 2020, kulikuwa na athari mbaya sana za kisaikolojia kwa serikali na jeshi la Afghanistan, kwani tayari walijua hakika tarehe ambayo watapoteza usaidizi wote wa kijeshi kutoka Marekani waliouzoea kwa miaka 20.

Soma zaidi:Taliban wataka kuzungumza katika baraza la Umoja wa Mataifa 

Katika makubaliano hayo ambayo yalisainiwa wakati wa utawala wa rais wa zamani Donald Trump, Marekani iliahidi kuondosha wanajeshi wake kuanzia mwezi Mei 2021, na kundi la Taliban likakubali kusimamisha mashambulizi dhidi ya vikosi vya Marekani na washirika wake.

Lengo kuu lilotajwa ilikuwa ni kukuza mazungumzo ya kutafuta amani kati ya Taliban na serikali ya Afghanistan, lakini juhudi hiyo ya kidiplomasia haikupata mvuto hadi pale Biden alipoingia madarakani mnamo mwezi Januari.

Kuanguka kwa serikali ya Afghanistan ulikuwa mkakati uliopangwa

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, aliekua akitoa ushuhuda pamoja na McKenzie amemuunga mkono kauli yake hiyo, na kusema makubaliano ya Doha yameahidi kutolishambulia tena kundi la Taliban na hivyo wanamgambo wake wakapata nguvu ya kuongeza mashambulizi dhidi ya vikosi vya serikali ya Aghanistan, ambavyo vilikuwa vikipoteza wanajeshi kila wiki.

DW Investigativ Special zum Thema LGBTQ Menschen nach der Machtübernahme durch die Taliban
Msafara wa wanamgambo wa kundi la Taliban, KabulPicha: Aamir Qureshi/AFP/Getty Images

Hata hivyo Jenerali Mark Milley, aliehojiwa mapema Jumanne katika kikao kama hicho mbele ya Seneti, amesema Marekani kutofaulu katika vita vya Afganistan ulikuwa ni mkakati uliopangwa, na alirudia tena kauli yake hiyo Jumatano.

Soma zaidi: Wito watolewa kwa EU kuongeza msaada nchini Afghanistan

Alipobanwa sana na kamati hiyo ya Seneti, Milley aliiambia kuwa maoni yake binafsi ni kwamba angalau wanajeshi 2,500 wa Kimarekani walihitajika kuilinda serikali ya Afghanistan isiporomoke.

Hivyo kukataliwa kwa tathmini za idara ya ujasusi ya Marekani, kulipelekea serikali ya Afghanistan na jeshi lake lililofunzwa na Marekani kuanguka katikati ya mwezi Agosti.

Na hapo ndipo kundi la Taliban, lilipopata fursa ya kuchukua udhibiti wa mji mkuu wa Kabul kwa kutumia wanamgambo mia moja tu waliokuwa kwenye pikipiki.

Mahojiano hayo ya Jumatano mbele ya kamati ya seneti yalikuwa na ushindani mkubwa wa kisiasa. Upande wa chama cha Republican ulikuwa ukitafuta sababu ya kumlaumu Biden kwa yaliotokea Afghanistan, na chama cha Democratic kilisema kuwa sababu ni maamuzi mabovu yaliyofanywa wakati wa utawala uliopita wa Trump.

Vyanzo: (ap,afp)