Taliban wataka kuzungumza katika baraza la Umoja wa Mataifa
22 Septemba 2021Katika barua hiyo ya Taliban kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, waziri wa mambo ya nje wa utawala wa kundi hilo Amir Khan Muttaqi ametaka haki ya kuzungumza katika mkutano wa baraza kuu wa 76 unaoendelea mjini New York. Barua hiyo ambayo shirika la habari la DPA limeona nakala yake, inatoa hoja kuwa rais wa Afghanistan Ashraf Ghani alikwishatumuliwa mamlakani, na kwa wakati huu hatambuliwi na taifa lolote.
Soma zaidi: Mjumbe wa UN Afghanistan aomba kubaki kwenye nafasi yake
Aidha, katika barua yake Taliban wamesema wanataka kumteuwa msemaji wa kundi hilo Suhail Shaheen kuwa balozi mpya wa Afghanistan katika Umoja wa Mataifa, akichukua nafasi ya Ghulam Isaczai ambaye kwa mujibu wa barua hiyo haiwakilishi nchi yoyote.
Taliban ambao walichukua hatamu za uongozi nchini Afghanistan mwezi uliopita wa Agosti, mamlaka yao yanatambuliwa na nchi nyingi za dunia kama Marekani na Ujerumani, ambazo hata hivyo hazitambui uhalali wa serikali waliyoiunda.
Waziri Mkuu wa Pakistan atoa onyo kwa Taliban
Wakati hayo yakiarifiwa, waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan ametoa onyo kwa Taliban, akisema Afghanistan itatumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ikiwa kundi hilo litashindwa kuunda serikali inayoyashirikisha makundi yote nchini humo.
Soma zaidi: Taliban yatangaza serikali mpya ya mpito Afghanistan
Huo ni ujumbe wa kwanza mkali kwa Taliban kutoka Pakistan, taifa ambalo limekuwa likituhumiwa kuliunga mkono kundi hilo. Imran Khan ambaye alikuwa akizungumza na idhaa ya Ki-urdu ya shirika la utangazaji la Uingereza, BBC, amesema iwapo Taliban hawatounda serikali ya wote, Afghanistan itakumbwa na vurugu, ambazo ni mazingira muafaka kwa makundi ya kigaidi.
Onyo la waziri mkuu Khan limetolewa wakati wajumbe wa Urusi, China na Pakistan wakifanya mkutano wa pamoja na utawala wa Taliban mjini Kabul, kwa lengo hilo hilo la kuwataka Taliban kuunda serikali jumuishi. Wajumbe hao maalumu wa nchi hizo majirani wa Afghanistan, walikutana pia na rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai, na mwanasiasa mashuhuri Abdullah Abdullah, hii ikiwa ni kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Pakistan.
Taliban wawili, raia mmoja wauawa Jalalabad
Habari zaidi kutoka Afghanistan zimearifu kuwa watu wenye silaha wamekishambulia kituo cha ukaguzi barabarani na kuwauwa wapiganaji wawili wa Taliban na raia mmoja. Shambulizi hilo limetokea katika mji wa Jalalabad kwenye mkoa wa Nangarhar, ambao kwa miaka mingi umekuwa ngome ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, tawi lake la Afghanistan.
dpae, afpe