1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Palestina inayotambulika itasaidia kumaliza mzozo Gaza?

14 Februari 2024

Hivi karibuni, miito ya kuyataka mataifa ya Magharibi kuitambua Palestina kama taifa imekuwa ikiongezeka, ijapokuwa Ujerumani haichukulii Palestina kama nchi, mataifa 139 kati ya 193 ya Umoja wa Mataifa yanaitambua.

https://p.dw.com/p/4cP03
Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Palestina Mohammad Shtayyeh
Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Palestina Mohammad Shtayyeh akizungumza katika mkutano wa Waandishi wa habariPicha: ZAIN JAAFAR/AFP/Getty Images

Hata hivyo, kilicho muhimu wakati huu, ni kwamba utambuzi huo unazingatiwa upya na Marekani, nchi ambayo awali ilipinga karibu kila jaribio la kuifanya Palestina kuwa nchi.

Mbali na Marekani, Uingereza pia inaonekana kufikiria kuhusu suala hilo ijapokuwa katika siku za nyuma, nchi hiyo imekuwa ikileta pingamizi kama vile Marekani.

Mapema mwezi huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Cameron, alisema kuwa kile wanachohitaji kufanya ni kuwapa watu wa Palestina fursa ya kuelekea katika mustakbali mwema wa kuwa na taifa lao.

Wanasiasa wakuu nchini Uhispania, Norway na Ireland, hivi karibuni pia wamezungumzia kuhusu uwezekano wa kuitambua Palestina kama taifa.

Hata hivyo, wataalamu wamehimiza tahadhari juu ya taarifa kutoka kwa Marekani na Uingereza, na kupendekeza kuwa kuna uwezekano zinatolewa ili tu kuiwekea shinikizo serikali ya Israel inayozidi kukaidi na kutobabaishwa na hatua ya washirika wake wanaoanza kutilia mashaka mbinu inazotumia katika Ukanda wa Gaza.

Soma pia:Ujumbe wa Israel waondoka Cairo bila ya kupatikana mafanikio

Ndiyo maana walipotakiwa kutoa ufafanuzi, wasemaji wa Marekani wamesema kuwa kwa sasa sera za serikali hazijabadilika.

Kwa nchi nyingi za Magharibi, wazo limekuwa kwamba mabadiliko ya hadhi ya Palestina yatakuja mwishoni mwa mazungumzo kuhusu kile kinachojulikana kama suluhisho la mataifa mawili, ambapo Israel na Palestina zitaishi kwa pamoja kama mataifa mawili huru.

Hii ndio maana kauli na tetesi za hivi karibuni zimezua mjadala mkubwa. Wengine wanasema kwamba kutambuliwa kwa Palestina kama taifa itakuwa hatua ya kwanza kuelekea suluhisho la kudumu na la amani kwa mzozo ambao umedumu kwa miongo kadhaa.

Lakini wengine wanasema kwamba ikiwa hali haitabadilika katika eneo hilo, kutambuliwa huko kutakosa maana na kuendelea kulifanya taifa la Israel kubaki na mamlaka yote.

Kuitambua Palestina kuna maanisha nini katika mzozo?

Kutambuliwa huko kutaipa Palestina nguvu zaidi ya kisiasa na kisheria na hasa uvamizi wa Israel au unyakuzi wa ardhi ya Palestina litakuwa suala kubwa zaidi la kisheria.

Josh Paul ambaye hadi hivi karibuni alikuwa mkurugenzi wa masuala ya bunge na umma katika ofisi ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani inayoshughulikia masuala ya kisiasa na kijeshi, lakini akajiuzulu kutokana na kutokubaliana kuhusu sera za Marekani kwa Gaza.

Ujumbe wa kupinga mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza
Ujumbe wa kupinga mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa GazaPicha: Michael M. Santiago/Getty Images

Amesema mabadiliko kama hayo, yataweka msingi wa mazungumzo ya hadhi ya kudumu kati ya Israeli na Palestina, sio kama orodha ya makubaliano kati ya wavamizi na waliokaliwa, lakini kati ya pande mbili ambazo ni sawa mbele ya sheria za kimataifa.

Philip Leech-Ngo, mchambuzi wa Mashariki ya Kati anayeishi Canada na mwandishi wa kitabu cha "Taifa la Palestina: Uchambuzi muhimu'', kilichochapishwa mwaka 2016, ameiambia DW kwamba labda faida kubwa zaidi kwa Palestina, hata hivyo, ni ya kiishara. Palestina huenda hatimaye ikaipeleka Israeli kwa mahakama ya kimataifa ya aina fulani, lakini hiyo itakuwa hatua ya siku za baadaye sana.
 "Hawawezi kuwapa Wapalestina zaidi ya kitu kingine chochote. Hawawezi kukabiliana na Israeli, hawana uwezo wa kuboresha maisha ya Wapalestina walio chini ya mamlaka yao na pia ni wafisadi na wasio na demokrasia. Kwa hivyo jambo pekee ambalo wanaweza kufanya ni ahadi ya kutambuliwa kimataifa.'' Alisema 

Soma pia:Israel yatahadharishwa dhidi ya kuanza kushambulia Rafah

Leech-Ngo ameendelea kusema kwamba mbali na yote, "kutambuliwa kama taifa itakuwa njia ya kusema kwamba jumuiya ya kimataifa inakubali kwamba suala la Palestina ni halali na katika mazingira ya kukaliwa kwa muda mrefu kwa maeneo yake na Israel, kunatoa faida kubwa ya kisiasa. 

Kura za maoni za hivi karibuni, zinaonyesha kuwa Waisraeli wengi hawataki kuiona Palestina kama taifa. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa akisema hivyo kwa miaka mingi. Na kwa Waisraeli na washirika wake wa kimataifa, pia kuna hofu kwamba ikiwa Palestina itatambuliwa kama taifa sasa, inaweza kuwa ushindi kwa wale wanaochochea ghasia.

Israel epusheni mauaji ya halaiki Gaza