1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaapa kumwangamiza kiongozi mpya wa Hamas

8 Agosti 2024

Israel imeapa kumwangamiza Kiongozi mpya wa Hamas na kusema imejiandaa kikamilifu kukabiliana na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran, huku hofu ikizidi kuongezeka kimataifa kuhusu kuzuka kwa vita vya kikanda.

https://p.dw.com/p/4jEyk
Benjamin Netanjahu na Kiongozi wa Hamnas, Yahya Sinwar (kulia)
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (kushoto) na Kiongozi mpya wa Hamas Yahya SinwarPicha: DEBBIE HILL/Pool via REUTERS/MAHMUD HAMS/AFP via Getty Images

Kiongozi mpya wa Hamas anayelengwa ni Yahya Sinwar aliyechaguliwa hivi majuzi na anayedaiwa kuwa mpangaji mkuu wa shambulio la Oktoba 7 mwaka jana kusini mwa Israel. Kauli hii inatolewa wakati uhasama kati ya Israel na Iran ukitishia kulitumbukiza eneo la Mashariki ya Kati kwenye vita vya kikanda huku mzozo wa Gaza ukiingia mwezi wa 11.

Kutangazwa kwa  Sinwar kuliongoza kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas, kumejiri wakati Israel ikijiandaa kukabiliana na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran kufuatia mauaji ya Ismail Haniyeh wiki iliyopita mjini Tehran.

Akizungumza katika kambi ya kijeshi hapo jana, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema Israel imedhamiria kujilinda na kwamba wako tayari pia kushambulia.

Israel inaendeleza mashambulizi katika Ukanda wa Gaza
Israel inaendeleza mashambulizi katika Ukanda wa GazaPicha: Bashar Taleb/AFP

Naye Mkuu wa jeshi la Israel Jenerali Herzi Halevi ameapa kumsaka na kumuangamiza Sinwar ili hatimaye kuwalazimisha Hamas kumtafuta mtu mwingine wa kuchukua nafasi yake.

Sinwar ambaye amekuwa kiongozi wa Hamas huko Gaza tangu mwaka 2017, hajaonekana hadharani tangu shambulio la Oktoba 7, ambalo lilikuwa baya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Israel. Afisa mkuu wa Hamas ameliambia shirika la habari la AFP kuwa uteuzi wa Sinwar ulituma ujumbe kwamba kundi hilo bado linaendelea na "harakati zao za ukombozi".

Soma pia: Marekani: Muhimu kuepusha vita kamili Mashariki ya Kati

Wachambuzi wanaamini kuwa Sinwar ana misimamo mikali zaidi na yuko karibu mno na Iran kuliko Haniyeh, ambaye alikuwa akiishi Qatar. Na pia Kiongozi huyo mpya wa Hamas alikuwa haafiki makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza.

Hezbollah yaapa kulipiza kisasi dhidi ya Israel

Kiongozi wa kundi la Hezbollah la huko Lebanon Hassan Nasrallah
Kiongozi wa kundi la Hezbollah la huko Lebanon Hassan NasrallahPicha: EPA/WAEL HAMZEH

Kiongozi wa kundi la Hezbollah la huko Lebanon Hassan Nasrallah ameapa kuwa watalipiza kisasi dhidi ya Israel kufuatia mauaji ya Kamanda wao Fuad Shukur mjini Beirut na hivyo kuzidisha hofu ya kuzuka kwa vita vya kikanda. Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant alijibu kauli ya kiongozi huyo wa Hezbollah na kusema:

" Kwa hali ya sasa ilivyo, Nasrallah anaweza kuisababishia Lebanon kulipa gharama kubwa mno. Yaani, hawawezi hata kufikiria ni nini kinachoweza kutokea. Nadhani wapige picha na kuiangalia  hali ya Gaza ndio wataelewa, lakini mara nyingi busara huwa inapuuzwa."

Soma pia: Blinken asema Sinwar anapaswa kusimamia makubaliano ya amani Gaza

Wiki hii Rais wa Marekani Joe Biden na yule wa Ufaransa Emmanuel Macron waliongea na viongozi wa Israel na Iran na kuwataka kujizuia na hatua zozote zinazoweza kuutanua mzozo huo. Rais mpya wa Iran Masoud Pezeshkian amesema ikiwa mataifa ya Magharibi yana nia ya dhati ya kutaka kuzuia vita, basi yanatakiwa kuacha kuiuzia silaha na kuiunga mkono Israel.

(Chanzo: AFP)