1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas yamteua Yahya Sinwar kuchukuwa nafasi ya Haniyeh

7 Agosti 2024

Hamas imemteua Yahya al-Sinwar kuchukuwa nafasi ya marehemu Ismail Haniyeh kama kiongozi mkuu wa kisiasa, wakati Mashariki ya Kati ikijiandaa kwa uwezekano wa wimbi la mashambulizi ya Iran na washirika dhidi ya Israel.

https://p.dw.com/p/4jCRh
Ukanda wa Gaza | Yahya Sinwar
Yahya Sinwar anashtumiwa na Israel kuwa kinara wa mashambulizi ya Oktoba 7.Picha: MAHMUD HAMS/AFP/Getty Images

Yahya Sinwar anashutumiwa na Israel kuwa kinara wa mashambulizi ya Oktoba 7 kusini mwa Israel, yaliowauwa takribani watu 1,200, wengi wao wakiwa raia, na kuwachukuwa mateka wengine wapatao 250.

Lakini licha ya mashambulizi ya angani na ardhini ya karibu miezi 10 dhidi ya Ukanda wa Gaza, Al-Sinwar amevikwepa vikosi vya Israel vinavyomsaka kwa udi na uvumba, huku akisema inaamini amejichimbia katika mahandaki ya chini ya ardhi ya ukanda huo wa Palestina.

Haniyeh aliyekuwa na makao yake nchini Qatar, aliuawa takribani wiki moja iliyopita katika shambulio la kulenga lililolaumiwa kwa Israel, wakati akiwa ziarani mjini Tehran kuhudhuria uapishwaji wa rais mpya wa Iran. Mauaji hayo yalifanyika siku moja baada ya Israel kumuuwa kamanda wa juu wa kijeshi wa kundi la Hezbollah Fuad Shukr mjini Beirut, nchini Lebanon.

Picha muunganiko| Benjamin Netanjahu na Yahya Sinwar
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kushoto, na kiongozi mpya wa Hamas, Yahya Sinwar, kulia, ni miongoni mwa walioombewa kibali cha kukamatwa na mahakama ya uhalifu wa kivita, ICCPicha: DEBBIE HILL/Pool via REUTERS/MAHMUD HAMS/AFP via Getty Images

Soma pia: Mwendesha mashtaka ICC aomba waranti dhidi ya Netanyahu, viongozi wa Hamas

Hofu ya kuzuka vita vikubwa vya kikanda imekuwa ikiongezeka wakati Iran na vikosi vyake washirika katika Kanda ya Mashariki ya Kati, ambavyo vinahusisha kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza, Hezbollah nchini Lebanon, na waasi wa Kihouthi nchini Yemen, wakiapa kulipiza kisasi juu ya mauaji hayo.

Al-Sinwar kuendeleza alipoishia Haniyeh?

Kuchaguliwa kwa Al-Sinwar mwenye usuhuba wa karibu na Iran na aliyetoa mchango mkubwa katika kuijenga Hamas, kunatazamwa kama ishara ya ukaidi kwamba kundi hilo limejiandaa kuendeleza mapambano baada ya vita vya muda mrefu na kuuawa kwa Haniyeh.

''Tunazingatia kwamba kuchaguliwa kwa Sinwar kunamaanisha uzinduzi mpya kwa ajili ya hatua mpya ambayo Sinwar atawasilisha, Mungu akipenda, na kutakuwa na mengi zaidi baada ya hatua hiyo, Mungu akipenda. Na tutawasilisha, kujitolea zaidi kwa ajili ya kuikomboa Palestina, Mungu akipenda,'' alisema Rabih Radwan, mwakilishi wa Hamas mjini Saida, nchini Lebanon.

Marekani | Mkutano maalumu wa Umoja wa Mataifa | Ombi la Palestina kuwa mwanachama kamili | Gilad Erdan
Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Gilad Erdan akionyesha picha ya Sinwar wakati wa kikao maalumu cha baraza la UN juhudi ya uanachama kamili wa Palestina wa UN, Aprili 18, 2024.Picha: Charly Triballeau/AFP/Getty Images

Tangazo la kuchaguliwa kwa Al-Sinwar limeibua hofu kwamba huenda likaikasirisha Israel na kuchochea vita zaidi, wakati viongozi wa juu wa Marekani wakiendelea na juhudi za kidiplomasia kuishinikiza nchi hiyo na Iran kuepusha mzozo mpana zaidi.

Soma pia:Netanyahu anasema jeshi la Israel limezingira makazi ya kiongozi wa Hamas 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, alisema hapo jana, katika matamshi yaliotafsiriwa kuwa yalioelekezwa zaidi moja kwa moja kwa Israel, kwamba hakuna anayepaswa kuchochea mzozo huo, na kubainisha kuwa Marekani imekuwa inafanya kazi kwa karibu na washirika kupunguza mzozo na kuepusha vita pana zaidi ya kikanda.

Blinken pia amepunguza athari za kuchaguliwa kwa mtu aliyeko kwenye orodha ya juu ya walengwa wa Israel, akisema Al-Sinwar ndiye amekuwa mwamuzi mkuu wa Hamas, na kuongeza kuwa kuchaguliwa kwake kunatilia tu mkazo ukweli kwamba ni juu yake kuamua kusonga mbele na usitishaji mapigano ambao utawasaidia Wapalestina wengi wenye uhitaji.

Chanzo: Mashirika