1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas yaitaka Marekani kuishinikiza Israel kusitisha vita

10 Juni 2024

Afisa mwandamizi wa Hamas ameitolewa wito Marekani kuishinikiza Israel kukomesha vita Gaza, kabla ya ziara ya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ili kuendeleza juhudi za usitishaji mapigano.

https://p.dw.com/p/4grnl
Rafah- Uharibifu uliotokana na mashambulizi ya Jeshi la Israel
Mpalestina akitembea katikati ya magofu huko GazaPicha: AP

Afisa huyo mwandamizi wa Hamas, Sami Abu Zuhri, ameutolea wito utawala wa Marekani kuzidisha shinikizo litakalowezesha kusitishwa kwa vita huko Gaza huku akisisitiza kuwa kundi hilo liko tayari kutathmini kwa nia njema mpango wowote utaofanikisha azma hiyo ya  kusitisha vita.

Kabla ya Blinken kuelekea Israel katika ziara yake ya nane eneo hilo, atafanya kwanza ziara nchini Misri kwa lengo la kuhakikisha kuwa vita hivi havitanuki hadi nchini Lebanon na anatazamiwa kukutana kwa mazungumzo na Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi mjini Cairo na baadaye wiki hii ataelekea pia Jordan na Qatar.

Soma pia: Mpango wa usitishaji vita Gaza kuamua hatma ya kisiasa ya Netanyahu

Mjini Tel-Aviv, Blinken atakutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ambaye anakabiliwa na shinikizo ndani na nje ya nchi yake kutokana na hatua zake katika vita hivi vya Gaza. Mjumbe wa baraza la mawaziri anayehusika na masuala ya vita Benny Gantz amejiuzulu jana Jumapili kutokana na mwenendo wa Netanyahu katika vita hivi.

Pendekezo la rais Biden la kuvimaliza vita Gaza

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: Vadim Ghirda/AP/dpa/picture alliance

Ziara ya Blinken inajiri baada ya Rais wa Marekani Joe Biden mwishoni mwa mwezi Mei, kutoa pendekezo la awamu tatu la kusitisha mapigano, kukomesha uhasama, kuachiliwa kwa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina, pamoja na mipango ya kuijenga upya Gaza baada ya vita.

Lakini Netanyahu hadi sasa hajaonesha nia ya kuafiki mpango huo na amekuwa kila mara akisema kuwa kamwe hatositisha vita Gaza kabla ya kulitokomeza kabisa kundi la Hamas. Lakini operesheni zake za kijeshi zimekuwa zikikosolewa mno hasa pale zinaposababisha maafa kwa raia.

Soma pia: Jeshi la Israel laishambulia miji ya Rafah na Nuseirat

Mwishoni mwa wiki iliyopita operesheni ya Israel ya kuwaokoa mateka wanne katika kambi ya al-Nuseirat huko Gaza ilisababisha vifo vya Wapalestina 274 huku wengine zaidi ya 700 wakijeruhiwa, idadi hii ikiwa ni kwa mujibu wa Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas. Operesheni hiyo pia iliwauwa mateka wengine watatu, mmoja wao akiwa na uraia wa Marekani, kwa mujibu wa video iliyosambazwa na tawi la kijeshi la Hamas.

Mahujaji waiombea amani Gaza

Saudi Arabia - Mahujaji wa Kiislamu wakijiandaa na ibada ya kila mwaka ya Hajj
Mahujaji wa Kiislamu ambao wameanza kuwasili mjini Makkah kujiandaa na ibada ya kila mwaka ya HajjPicha: Abdel Ghani Bashir/AFP

Mahujaji wa Kiislamu ambao wameanza kuwasili mjini Makkah kujiandaa na ibada ya kila mwaka ya Hajj, wameomba kusitishwa kwa mapigano huko Gaza kama anavyoeleza Alia Asmaa.

"Kwa kweli inasikitisha sana kuona kile kinachotokea kila siku huko Gaza. Na tunaudhika kabisa. Tuna hisia ya kutoweza kufanya chochote kwa vitendo. Siku zote sala zetu tunazielekeza Gaza na inasikitisha mno kuona watu wanakufa kila siku. Matarajio yangu kwa  Gaza ni kuona vita hivi vinakomeshwa haraka na maisha ya watu yaokolewe na kutoshuhudia tena vifo. Kwa hivyo tunachotaka ni usitishwaji mara moja wa mapigano na ndio nilivyoomba jana wakati nilipokuwa nafanya ibada yangu ya umrah."

Wakati vita vikiendelea, ndege ya mizigo ya Marekani ilidondosha hapo jana zaidi ya tani 10 za msaada wa chakula kaskazini mwa ukanda wa Gaza.

(Vyanzo: Mashirika)