1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa usitishaji vita na hatma ya kisiasa ya Netanyahu

Angela Mdungu
4 Juni 2024

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anakabiliwa na shinikizo kubwa la kimataifa linalomtaka kukubaliana na mpango wa usitishaji vita na kuachiliwa kwa mateka katika mzozo wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4gdRR
Benjamin Netanyahu akiongoza baraza la mawaziri Januari 22, 2023
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Maya Alleruzzo/AP/dpa/picture alliance

Hayo yanajiri wakati upinzani ndani ya serikali yake ya mseto ukimaanisha kuwa huenda nafasi yake kisiasa ipo mashakani.Washirika wa Netanyahu wanaofuata siasa kali za mrengo wa kulia wametishia kujiondoa katika serikali baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuwasilisha pendekezo la mpango wa kusitisha vita.

Hali hii inamfanya Netanyahu kuvitegemea vyama vinavyofuata siasa za wastani ambavyo navyo vinasubiri kutumia nafasi yoyote vitakayoipata kumuondoa madarakani.

Jumamosi iliyopita, maelfu ya Waisraeli waliandamana kumtaka akubaliane na mpango huo wa kuwaachilia mateka wanaoshikiliwa na Hamas Ukanda wa Gaza. Kulingana na taarifa za jeshi, kundi hilo liliwateka watu 251 Oktoba 7 kutoka Israel na kati ya hao 120 bado wanashikiliwa Gaza na 41 miongoni mwao wameshauwawa.

Soma zaidi: Kiongozi wa upinzani Israel amtaka Netanyahu kuzingatia mpango wa kusitisha mapigano Gaza

Maandamano kama hayo yamekuwa yakifanyika kila mwisho wa juma kwa miezi kadhaa sasa lakini maandamano ya Jumamosi yalikuwa tofauti baada ya Biden kuwasilisha mpango huo. Hata hivyo Netanyahu alizima haraka matumaini kwa kusema kuwa masharti ya mpango wa Biden hayakuwa na mabadiliko na wala hayakujumuisha kile alichokiita "kulisambaratisha"  kundi la Hamas.

Waandamaanaji wa Israel wanataka mateka wanaoshikiliwa na kundi la Hamas waachiliwe
Maandamano dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Mahmoud Illean/AP/picture alliance

Mtaalamu wa sayansi ya siasa katika chuo cha Kiebrania cha Jerusalem Profesa, Gideon Rahat anasema huenda Netanyahu akawa na majibu yasiyokubalika kwa sababu ya maslahi yake binafsi ya kisiasa.

Washirika muhimu wanavyotishia kujiondoa katika serikali ya mseto

Washirika wa waziri mkuu huyo wa Israel, Waziri wa Usalama wa Taifa Itamar Ben Gvir na Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich wametishia kujiondoa kwenye serikali ya mseto kama Netanyahu ataamua kusitisha vita kabla ya kuiangamiza Hamas. Serikali yake ya pamoja inaongoza taifa hilo kwa viti vichache 64 kati ya 120 vya bunge na inategemea kura za mrengo wa kulia.

Kwa upande wake mtaalamu wa siasa wa chuo cha Bar Ilan, Ilan Greilsammer anadhani kuwa kama makubaliano ni kusimamisha haraka mapigano na kuwarejesha nyumbani wanajeshi, ni vigumu kufikiri ikiwa washirika hao watasalia serikalini.

Greilsammer  anaongeza kuwa kama wanasiasa wa mrengo wa kulia hawatajiengua kwenye serikali, njia pekee ya Netanyahu kurejea kwenye serikali yenye viti vingi bungeni itakuwa kupitia makubaliano na chama cha upinzani chake Yair Lapid kinachofuata siasa za wastani cha Yesh Atid.

Yair Lapid
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Yeah Atid cha Israel, Yair LapidPicha: Ohad Zwigenberg/AP/picture alliance

Soma zaidi: Pendekezo la kumaliza vita Gaza laitikisa serikali ya Israel

Tayari chama hicho kilishaonesha utayari wa kumuunga mkono ili kupata makubaliano ya kuwarejesha mateka. Kuna mashaka kuwa, uungaji mkono huo huenda ukawa wa muda mfupi tu ukiibua maswali juu ya hatma ya kisiasa ya waziri mkuu huyo wa Israel.

Kwa upande wake Mtaalamu wa siasa Denis Chabit wa Chuo huria cha Israel anasema kuna uwezekano mkubwa wa washirika wa Netanyahu kumkimbia serikalini. Anaongeza kuwa si rahisi kwa chama cha National Unity cha Waziri katika  baraza la mawaziri la vita la Israel Benny Gantz kujiunga na serikali yake kigezo kikubwa kikiwa ni iwapo uchaguzi wa mapema utaitishwa au la.

Gantz alijiunga na baraza hilo baada ya shambulio lililofanywa na Hamas ndani ya Israel Oktoba 7 lakini chama chake hakijajiunga na serikali ya mseto. Mwezi uliopita, alitishia kujiuzulu katika baraza hilo kama Netanyahu asipoidhinisha mpango wa namna ya kuiongoza Gaza baada ya vita. Wiki iliyopita, chama chake kiliwasilisha muswada wa kulivunja bunge na kutaka uitishwe uchaguzi wa mapema.

Kulingana na kura ya maoni iliyoendeshwa na televisheni ya umma ya Israel, asilimia 38 ya wapiga kura wa Israel wanahisi kuwa Gantz anafaa kuwa Waziri Mkuu, wakati Netanyahu alipata asilimia 30 pekee.