Israel yawaokoa mateka wanne wakiwa hai huko Gaza
8 Juni 2024Jukwaa linalowaunganisha ndugu na jamaa wa mateka wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza lilipongeza uokoaji wa mateka hao wanne kutoka kwenye ardhi ya Palestina siku ya Jumamosi.
Jukwaa hilo limesema: "Operesheni ya kishujaa ya jeshi la Israel ambayo iliwezesha kuokolewa kwa Noa Argamani, Shlomi Ziv, Andrey Kozlov, na Almog Meir Jan ni ushindi wa kimiujiza," na kuongeza kwamba wanaendeleza juhudi kwa jumuiya ya kimataifa ili kuishinikiza Hamas kuwaachilia mateka wengine.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema siku ya Jumamosi kuwa Israel haitozuiliwa na ugaidi na kwamba itaendelea na operesheni yake "kwa ubunifu na ushujaa" ili kuwarejesha nyumbani mateka wote wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza.
"Tumejitolea kufanya hivyo katika siku zijazo pia. Tutafanya hivyo na hatutokata tamaa hadi tukamilishe azma yetu ya kuwarejesha nyumbani mateka wote ima wawe hai au wamekufa," Netanyahu alisisitiza.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema taarifa ya kuokolewa mateka wanne wa Israel ni ishara yenye kuleta matumaini.
Hamas: Israel haiwezi kutulazimisha chochote
Hata hivyo Kiongozi wa Kundi la Hamas Ismail Haniyeh amesema kamwe Israel haiwezi kuwalazimisha matakwa yao na kuwa kamwe hawatoafiki makubaliano yoyote ambayo hayatozingatia usalama kamili wa Wapalestina.
Soma pia: Mpango wa Biden wa kusitisha mapigano Gaza bado kizungumkuti
Haniyeh ameitoa kauli hiyo kujibu tukio la hivi karibuni zaidi la jeshi la Israel kulishambulia eneo la al-Nuseirat katika Ukanda wa Gaza ambako hadi sasa inaarifiwa kuwa watu wasiopungua 55 waliuawa. Israel ilidai kuwa mateka wawili kati ya wanne waliookolewa walipatikana eneo hilo la al-Nuseirat.
Mamlaka za Hamas, ambayo imeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa kadhaa ya Magharibi kama kundi la kigaidi zimesema watu waliouawa katika shambulio la Israel huko Nuseirat imefikia 93.
Katika taarifa yake, Haniyeh amesema: " Watu wetu kamwe hawatajisalimisha na wataendelea kupambana na kutetea haki zao dhidi ya adui huyu mhalifu. Ikiwa wavamizi wa Israel wanadhani kwamba wanaweza kutulazimisha matakwa yao kwa kutumia mabavu, basi wanajidanganya kabisa."
Soma pia: Israel yaishambulia Rafah licha ya uamuzi wa ICJ
Israel imeendeleza mashambulizi yake huko Gaza na kujikita zaidi katika eneo la katikati mwa Ukanda huo. Hayo yanajiri licha ya Israel kulaumiwa baada ya kuishambulia shule inayosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).
Serikali mjini Tel-Aviv imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji mkubwa kufuatia mashambulizi yake katika maeneo ya makazi ya raia, kambi za wakimbizi na hata shule. Waziri wa Israel anayehusika na mikakati ya vita ametishia kujiuzulu baada ya kuongezeka kwa shinikizo kubwa kutokana na mwenendo wa nchi yake katika operesheni ya kijeshi huko Gaza ambayo hadi sasa kulingana na Wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas, tayari imesababisha vifo vya Wapalistina zaidi ya 36,000.
Vyanzo: Mashirika