1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya maisha ya wahamiaji nchini Ureno

Lillian Urio4 Agosti 2005

Ureno ni taifa mojawapo la Ulaya ambalo watu wengi kutoka nchi zinazoendelea wanapenda kuhamia. Kati ya wananchi wa Ureno kumi, moja si mzaliwa wa nchi hiyo. Wahamiaji walizidi kwenda Ureno baada ya nchi hiyo kujiunga na Jumuiya ya Ualya, na hivyo kuifanya muhimu zaidi ,kisiasa na kiuchumi.

https://p.dw.com/p/CHfS
Lisbon, mji Mkuu wa Ureno
Lisbon, mji Mkuu wa UrenoPicha: AP

Watu wengi wanaohamia Ureno wanatoka nchi zilizo kuwa makoloni ya zamani ya Ureno, mfano Angola na Cape verde. Lakini ni wachache kati yao wanaohisi wanajumuishwa kikamilifu katika jamii za Kireno.

Wawakilisha wa shirika la wahamiaji nchini humo wanasema sera za uhamiaji za nchi hiyo hazieleweki vizuri, kwa hiyo ni shida kuzifuatilia.

Kwa mujibu wa msemaji wa shirikisho la jumiya za

wahamiaji wanaozungumza Kifaransa, Mamadou Ba, sera hizo zimetokana na mkusanyiko ya sheria tofauti kutoka serikali za Ureno, katika kipindi cha miaka kumi.

Anasema masuala juu ya elimu, huduma za afya na kazi hayajawahi kufanyiwa marekebisho kabisa. Kama watayashughulika basi itasaidia katika kuwajumuisha wahamiaji kwenye jamii. Wananchi kutoka nje wanatengwa, hasa wale kutoka nchi Ureno ilizozimiliki wakati wa ukoloni, za Angola na Cape Verde.

Mfanya biashara Cady Indjai kutoka Guinea-Bissau amekuwa akiishi Ureno kwa miaka minane sasa na anajihisi vizuri nchini humo, wakati mume wake anaishi Kanada na watoto wake Ufaransa. Lakini anasema akiona matatizo yanayoyowapata wengine, kupitia televisheni, anaona kwamba serikali haiwajali.

Serikali ya Waziri Mkuu Jose Socrates imependekeza sheria mypa inayolenga kuwasaidia wageni katika masuala ya kijamii, hasa kwa wale waliopoteza ajira.

Yaya Djalo amekuwa akiishi nchini Ureno kwa miaka mitano na alikuwa akifanya kazi kwenye sekta ya ujenzi. Ameacha familia yake Guinea-Bissau, na kama atapewa kibali kingine cha kufanya kazi, kwa kipindi cha miaka mitano, basi ataileta familia yake.

Maisha ya mhamiaji ni yale ya kukumbuka sana nyumbani na kuhangaika kuinua hali ya maisha. Lakini hata watoto wa wahamiaji wanaozaliwa Ureno wanabaguliwa.

Kwa maoni ya Bwana Djalo, wazazi na walezi wanafanya kazi sana, kwa hiyo mara nyingi watoto wanaachwa nyumbani peke yao. Inawabidi wazazi wafanye hivyo sababu hawana fedha za kutosha kuwapeleka watoto kwenye vituo vya kulea watoto vya mchana. Watoto hao wanakua bila kulelewa vizuri na baadae wakiwa watu wazima wanakuwa na matatizo yanayowafanya wasikubalike vizuri katika jamii.

Watoto wa wahamiaji na wajukuu wao hawana haki ya uraia wa Ureno, hata kama wamezaliwa nchini humo. Wengine hawana hata vibali halali vya kuishi nchini.

Tatizo lingine ni lugha, hasa kwa wahamiaji kutoka nchi za Afrika zinazozungumza Kifaransa au Kiingereza wanapata shida zaidi.

Kwa maoni ya Djalo Mamadou aliyeishi Ureno kwa kipindi cha miaka sita anaona ni vigumu sana kwa wahamiaji kushiriki kikamilifu kwenye jamii. Wakati mwingine mshahara wake unacheleweshwa kwa mwezi moja au miwili.

Bwana Mamadou anasema tatizo lingine la mhamiaji ni kukaa mbali na familia yake. Inambidi amtumie mke wake fedha kila mara. Angependa kumleta mke wake lakini hawezi kwa sababu hali ya maisha haimuruhusu.

Alidhani akihamia Ureno basi maisha yake yatakuwa mazuri, lakini leo hii anaona maisha ya Ulaya kama adhabu. Anawaza kurudi nyumbani, lakini anaona bila ya fedha za kutosha hawezi kufanya hivyo, na sasa hivi ameshaichoka nchi ya Ureno.

Sheria hiyo mpya ya wahamiaji pia inataka kuwajumuisha zaidi katika masuala ya kisiasa. Itawapa wahamiaji haki ya kupiga kura baada ya kuishi nchini humo kwa kipindi watakacho kitaja. Lakini je mapendekezo haya yatawasaidia na kuwafurahisha wahamiaji?

Mamude Djalo kutoka Guinea-Conakry ameishi Ureno kwa kipindi cha miaka mitano na anadhani suala muhimu ni kazi. Anasema wanafanya kazi katika mazingira magumu kwa malipo madogo. Wakati huo huo ni vigumu kumudu maisha ya kila siku. Pia ni vigumu kwa wahamiaji kununua tiketi ya ndege kwenda kuzitembelea familia Afrika.

Kwa hiyo wanasubiri kuona hali itakuwaje hapo baadae kabla hawaja furahia hiyo sheria mypa.