1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haki ya mazingira kuanzishwa

Josephat Charo15 Mei 2007

Mada mpya iitwayo ´haki ya mazingira´ inaukabili mjadala juu ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Mwandishi wetu Monika Hoegen anaripoti juu ya mjadala wa mazingira unaondelea.

https://p.dw.com/p/CHkw
Klaus Töpfer, mkurugenzi wa zamani wa shirika la UNEP
Klaus Töpfer, mkurugenzi wa zamani wa shirika la UNEPPicha: AP

Wananchi wa mataifa maskini duniani wanateseka kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa zinazosababishwa na mataifa yaliyoendelea zaidi kiviwanda. Hali hii haitakiwi kuendelea kubakia hivyo. Mataifa yanayoendelea yanatakiwa yasaidiwe kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake.

Lakini ukweli ulio wazi ni kuwa haijulikani vipi swala hilo litakavyotekelezwa na ni nani anayetakiwa kushtakiwa kwa kusababisha mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa hivyo jambo hilo limeendelea kubakia kuwa kitendawili cha kimataifa ambacho hakijapata ufumbuzi.

Je haki ya mazingira ya kimataifa ina maana gani? Klaus Töpfer, waziri wa zamani wa mazingira wa Ujerumani aliyekuwa pia zamani mkurugenzi wa shirika la mazingira la Umoja wa Matiafa, UNEP, ametoa mwito bara la Afrika liangaliwe kw mtazamo mpya ambao hauzungumzii tu ushirikiano wa kimaendeleo au misaada ya kifedha bali jukumu la kuhakikisha usawa na mabara mengine.

´Tunachokifanya kwa ajili ya Afrika hakihusiana na utoaji wa misaada bali azma ya kutaka hatimaye kulipa kwa juhudi zinazofanywa na bara la Afrika pamoja na Waafrika kwa ajili ya dunia. Hilo ndilo lengo.´

Maneno ya Töpfer yanafaa hususan katika swala la ulimwengu na mazingira kwa sababu nchi za kiafrika na mataifa yanayoendelea kwa jumla yanakabiliwa na hatari ya kunyanyaswa bila mipaka.

´Tunatarajia mazungumzo yanayounga mkono misitu katika nchi za joto ibakie ilivyo, na hatuko tayari kulipa hata senti moja, tukifahamu kwamba misitu hii inahifadhi kiwango kikubwa cha gesi ya carbon dioxide duniani, ambayo bila hiyo tungekuwa tayari kwa muda mrefu tunakabiliwa na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa.´

Hivyo ndivyo wanavyofikiri wajumbe wengine ambao wanataka kuanzisha muungano mpya wa kimataifa kuhusu mazingira. Wanasema nchi zinazoendelea zinakabiliwa na majanga ya kiasili lakini wakati huo huo zinateseka kutokana na unyanyasaji wa kimazingira, ambao haudhihiriki katika mabadiliko ya hali ya hewa. Hivyo nchi hizo haziteseki kwa makosa yao bali mataifa yaliyoendelea yanabeba dhamana kwa athari za kimazingira.

Meena Raman, wakili na mwanaharati kutoka Malaysia ambaye pia ni mwenyekiti wa shirika la kimataifa la kuyalinda mazingira la ´Friends of the Earth´ anataka kuwepo na haki ya mazingira.

´Kuhusu mjadala wa mazingira, shirika la kimataifa la ´Friends of the Earth´ limeanzisha mpango wa haki ya mazingira, ambapo tunazisaidia jamii kuzishitaki serikali ambazo hazichukui hatua. Kwa mfano tunajua kuna jamii nchini Bangladesh ambazo zimeanza kufikiria kuzichukulia hatua serikali za kaskazini kwa kutofanya lolote kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa na kuongeza kwa kiwango cha maji baharini.´

Wanaharati wa mazingira na wajumbe wa asasi zisizo za kiserikali ulimwenguni kote wanasema ipo haja ya kuibadili hali inazoyakabili mataifa yanayoendelea kutokana na athari za kimazingira. Idadi kubwa ya watetezi wameungana pamoja kupigania haki ya mazingira.