1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gueterres akosoa sera ya wakimbizi

Mohammed AbdulRahman8 Juni 2006

Anasema hatua zinazochukuliwa ni kitisho kwa historia ndefu ya kuwapa hifadhi wenye kuhitaji kweli kinga.

https://p.dw.com/p/CHn9
Wakimbizi kutoka Afrika walioingia katika visiwa vya Canary.
Wakimbizi kutoka Afrika walioingia katika visiwa vya Canary.Picha: AP

Kamishna mkuu wa Shirika la wakimbizi wa Umoja wa mataifa Antonio Gueterres alisema hayo yamesababisha hatua za vipingamizi zaidi kuhusiana na sera za kuheshimu hifadhi ya mazingira.

Bw Gueterres ambaye ni waziri mkuu wa zamani wa Ureno, anayemaliza mwaka wake wa kwanza katika wadhifa huo kama Kamishna mkuu wa shirika la wakimbizi la umoja wa mataifa, alisema kuna fikrana maoni tafauti miongoni mwa umma wa ulaya kati ya wahamiaji wa kiuchumi wanaoelekea Ulaya kutafuta maisha bora na wale wanaokimbia ukandamizaji na hatua za kuandamwa katika nchi zao.

Alisema wasi wasi mkubwa ni maoni ya umma kwani kunaonekana kuna hali ya kukosekana haja ya kutambua matatizo ya wakimbizi na watu kutoelewa haja ya kuwalinda wale wanaohitaji kinga .

Hata hivyo Bw Gueterres hakuishutumu serikali ya nchi yoyote ya Ulaya., lakini anahofia kunaweza kukaweko na kesi fulani za watu wanaohitaji kweli kinga kama wakimbizi na wakakataliwa.

Bw Gueterres amekua na mawasiliano na serikali ya Uhispania, ambako picha za televisheni kila siku huonyesha mashua ndogo zikiwa zimejazana waafrika wanaowasili katika visiwa vya Kanari, na kuzusha hasira za umma juu ya wimbi la uvamizi wa wahamiaji. Lengo lake lilikua ni kuhakikisha wakimbizi wanaelewa haki zao. Alisema wengi ni wahamiaji wa kiuchumi waokuja katika maeneo mengine ya dunia lakini kuna idadi ya wachache ambao kweli wanahitaji kinga ya kimataifa.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa shirika la wakimbizi la umoja wa mataifa, suluhisho la suala la wahamiaji linahitaji hatua za pamoja. Hizo ni pamoja na msaada wa kiuchumi kushajiisha maendeleo katika nchi wanakotoka, kusaidia kuendeleza mifumo ya kuwasaidia wakimbizi katika nchi wanakopita na sera bora kushajiisha kujumuishwa katika jamii kwa wahamiaji katika nchi za Ulaya.

Wananchi katika nchi tajiri pia wanahitaji ni kufahamu kwamba wengi miongoni mwa wakimbizi wanataka hifadhi, hupendelea kurudi makwao haraka mara tu kitisho kinapoondoka.

Katika mwaka uliopita, Shirika la wakimbizi la umoja wa mataifa, limewasaidia zaidi ya wakimbizi milioni moja kurudi makwao katika nchi kama Afghanistan, Liberia, Angola na Burundi ambako mara nyingi maisha yamekua bado ni magumu kwao.

Bw Gueterres alisema lengo lao sio Ulaya au Marekani bali kurudi nyumbani na wanaonyesha hamu kubwa ya kufanya hivyo, ili mradi tu kuna usalama.

Ingawa idadi ya wakimbizi imeendelea kupungua kutokana na kupungua kwa migogoro mikubwa duniani, Shirika la wakimbizi la Umoja wa mataifa, lina jukumu pia la kuwahudumia waliotawanyika na kuyahama makaazi yao ndani katika nchi zao ambao idadi yao imekua ikiongezeka.

Mzozo wa jimbo la Sudan la Darfur na Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo ndiyo inayoshika bendera na wasi wasi mkubwa katika tatizo hilo, lakini fedha zinazohitajika kuwasaidia mamilioni ni shida kupatikana na Bw Gueterres anasema » hakufikiria kama atalazimika kutumia muda wake mwingi kutafuta fedha tu. »