1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia zaendelea Ufaransa

1 Julai 2023

Ghasia zilizoibuka zimeendelea kwenye miji kadhaa ya Ufaransa kwa usiku wa nne mfululizo kutokana na mauaji ya kijana mwenye miaka 17 yaliyofanywa na polisi wa usalama barabarani.

https://p.dw.com/p/4TIo6
Frankreich, Bordeaux | Anhaltende Protete und Ausschreitungen nach dem Tod des 17-jährigen Nahel
Picha: Guillaume Bonnaud/SUD OUEST//MAXPPP/dpa/picture alliance

Zaidi ya watu 1,300 wamekamatwa, licha ya ulinzi mkali na kufungwa kwa huduma za usafiri wa umma. Hayo yanajiri wakati marafiki na familia wakifanya maziko ya kijana huyo Jumamosi.

Waziri wa mambo ya ndani Gérald Darmanin amewaambia waandishi wa habari mapema  Jumamosi kuwa licha ya matukio ya uporaji, uharibifu wa mali na makabiliano na polisi, vurugu zimepungua ikilinganishwa na Alhamisi usiku. Darmanin amesema zaidi ya magari 1,350 yamechomwa moto na kuna idadi ya visa 2,560 vya moto ulioanzishwa kwenye barabara za umma. 

Soma zaidi: Hamkani bado si shwari Ufaransa kufuatia kifo cha Nahel

Uharibifu umeshuhudiwa zaidi Paris, Marseille, Lyon, na hata  maeneo yaliyo chini ya utawala wa Ufaransa, nje ya taifa hilo ambapo kwa upande wa Guiana, mwanamume wa miaka 54 ameuwawa baada ya kupigwa risasi.

Polisi wakikabiliana na waandamanaji mjini Paris, Ufaransa
Polisi wakikabiliana na waandamanaji mjini Paris, UfaransaPicha: Firas Abdullah/AA/picture alliance

Mamlaka za Ufaransa zimesema takribani maafisa wa polisi 150 wamejeruhiwa wakati wa ghasia za Ijumaa usiku. Vikosi maalumu ni kati ya maafisa usalama 45,000, waliosambazwa kudhibiti maandamano.

Ili kukomesha vurugu, waziri wamambo ya ndani, Darmanin alisimamisha safari za mabasi na treni kote nchini humo kuanzia saa tatu usiku, hadi itakapotangazwa tena.

Waendesha mashtaka walianzisha uchunguzi rasmi wa mauaji ya bila kukusudia dhidi ya afisa wa polisi anayedaiwa kuwa alimfyatulia risasi kijana huyo aliyejulikana kwa jina la Nahel huko Nanterre.

Macron aahirisha ziara yake Ujerumani kushughulikia vurugu

Katika hatua nyingine, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameahirisha ziara yake nchini Ujerumani ili kushughulikia vurugu zinazoendelea nchini mwake kwa usiku wa nne mfululizo.

Ofisi ya rais wa Ujerumani imetangaza kuwa Macron amezungumza kwa njia ya simu na Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na kumfahamisha kuhusu hali nchini mwake, wakati akiomba ziara yake iliyopangwa kuanza Jumapili iahirishwe. 

Mapema Ijumaa Rais Macron, aliitisha kikao cha dharura kufuatia vurugu zilizojitokeza. Kinyume na ilivyotarajiwa na wengi, Macron hakutangaza hali ya dharura lakini alitoa wito kwa wazazi kuwaasa vijana wao wasishiriki kwenye maandamano ya vurugu

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: LUDOVIC MARIN/AFP

Timu ya soka ya Ufaransa imetoa wito wa kukomeshwa kwa machafuko. Katika kauli ya hiyo wachezaji wamesema kuwa vurugu hazitatui tatizo lolote na kwamba kuna njia nyingine za amani za watu kuonesha hisia zao. Timu hiyo imesema ni wakati wa kuomboleza, na kufanya mazungumzo

Mama wa kijana Nahel aliyeuwawa aliyejitambulisha kwa jina la Mounia M. ambaye familia yake ina asili ya Algeria, alikiambia kituo cha televisheni cha France 5 kuwa ana hasira na afisa wa polisi aliyemuua mwanaye lakini si kwa jeshi zima.