1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FBI yasema Trump alilengwa katika jaribio la mauaji

16 Septemba 2024

Milio y risasi imeripotiwa karibu na uwanja wa gofu wa Donald Trump wakati mgombea urais huyo akicheza gofu Jumapili. Rais huyo wa zamani ameripotiwa kuwa salaama.

https://p.dw.com/p/4keJB
Marekani| Donald J. Trump
Secret Service inasema Trump alilengwa katika jaribio la mauajiPicha: Kyle Mazza/NurPhoto/picture alliance

Maafisa wa idara ya ulinzi wa viongozi, Secret Service walifyatua risasi baada ya kumuona mtu akiwa na bunduki karibu na klabu ya gofu ya Trump ya West Palm Beach huko Florida wakati mgombea huyo wa urais wa chama cha Republican akicheza gofu.

Hakuna majeraha yaliyoripotiwa. Maafisa wanasema mtu huyo alikimbia kwa kutumia gari aina ya SUV na baadaye akakamatwa na vyombo vya sheria vya eneo hilo.

Soma pia: Donald Trump yuko salama baada ya "jaribio la kuuawa."

Haijabainika mara moja ikiwa risasi zilizoripotiwa zilimlenga Trump. Secret Service ilisema inachunguza na kwamba tukio hilo lilitokea muda mfupi kabla ya saa 2 usiku. "Rais wa zamani yuko salama," kulingana na kikosi hicho cha ulinzi wa viongozi.

Takriban miezi miwili iliyopita, Trump alipigwa risasi wakati wa jaribio la kumuua kwenye mkutano huko Pennsylvania, na risasi ikashika sikio lake.

Marekani, Las Vegas|  Trump | Timu ya maafisa wa Secret Service
Wanachama wa Timu ya kupambana na mashambulizi ya Secret Service wakipanda ndege baada ya kampeni ya mgombea urais wa Republican Donald Trump kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Harry Reid baada ya safari ya kampeni, Jumamosi, Septemba 14, 2024, Las Vegas.Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Mkuu wa polisi wa Kaunti ya Palm Beach, Ric Bradshaw, amesema mtu ambaye alinyooshea bunduki kwenye uzio kwenye uwanja wa gofu wa Trump alikuwa karibu yadi 400-500 kutoka kwa rais huyo wa zamani na alikuwa amejificha kwenye vichaka huku rais huyo wa zamani akicheza gofu kwenye shimo la karibu.

Mwanamume huyo alikuwa na bunduki aina ya AK yenye kifaa cha kulenga shabaha, mikoba miwili ikining'inia kwenye uzio na kamera ya GoPro, alisema Bradshaw. Mtu huyo alidondosha silaha yake na kukimbilia kwenye gari kabla ya kukamatwa katika kaunti jirani.

Soma pia: Harris amkaanga Trump kwenye mdahalo wa televisheni

Sherifu wa Kaunti hiyo ya Martin, William Snyder aliambia WPTV kwamba mshukiwa anaeaminika kuhusishwa na tukio hilo "hakuwa na silaha tulipomtoa kwenye gari."

Trump alirejeshwa salama baada ya tukio hilo kwenye klabu yake ya kibinafsi ya Mar-a-Lago, ambako anaishi katika eneo jirani la Palm Beach, kulingana na mtu anayefahamu suala hilo.

Mwanamume huyo alikuwa mtulivu, mwenye tabia nyororo na alionyesha hisia kidogo aliposimamishwa na polisi, Snyder alisema, na kuongeza kuwa mshukiwa hakuhoji kwa nini alikuwa anasimamishwa.

Kuwasili Las Vegas| Donald Trump
Mgombea urais wa chama cha Republican Rais wa zamani Donald Trump akiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Harry Reid ili kupanda ndege baada ya safari ya kampeni, Jumamosi, Septemba 14, 2024, Las Vegas.Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

"Hakuwahi kuuliza, 'Hii inahusu nini?' "Ni wazi, wasimamizi wa sheria walio na bunduki ndefu, taa za bluu, mengi yanaendelea. Hakuwahi kuhoji," Snyder alisema.

Trump awaambia wafuasi wake: Kamwe sintojisalimisha

Katika barua pepe kwa wafuasi wake, Trump alisema: "Kulikuwa na milio ya risasi karibu yangu, lakini kabla ya uvumi kuanza kuenea nje ya udhibiti, nilitaka msikie hili kwanza: NIKO SALAMA NA MWENYE AFYA!"

"Hakuna kitakachonipunguza kasi. SITAJISALIMISHA KAMWE!" rais huyo wa zamani alisema.

Secret Service ilisema imeanzisha uchunguzi na kwamba tukio hilo lilitokea muda mfupi kabla ya saa nane mchana (saa za Marekani). "Rais wa zamani yuko salaama," kwa mujibu wa Secret Service.

Ikulu ya White House ilisema Rais Joe Biden na Makamu wa Rais Kamala Harris, mgombea urais wa chama cha Democratic walikuwa wote wamearifiwa na wataendelea kupewa taarifa kuhusu uchunguzi. Ikulu ya White House iliongeza kwamba "wamefarijika" kujua Trump yuko salaama.

Afisa mmoja wa sheria ambaye hakutaka jina lake litajwe kuzungumzia uchunguzi unaoendelea alisema maafisa walikuwa wakijaribu kubaini iwapo risasi hizo zilifyatuliwa karibu na uwanja wa gofu wa Trump wa West Palm Beach au kwenye uwanja huo.

Marekani, Florida West Palm Beach| Risasi karibu na Trump
Afisa wa polisi akionyesha ishara wakati wakichunguza ripoti za risasi zilizofyatuliwa nje ya uwanja wa gofu wa mgombea urais wa chama cha Republican na aliyekuwa Marekani Donald Trump huko West Palm Beach, Florida, Marekani, Septemba 15, 2024.Picha: Marco Bello/REUTERS

Afisa huyo hakuidhinishwa kuzungumza hadharani na alizungumza na The Associated Press kwa sharti la kutotajwa jina.

Trump amepangiwa kuzungumza mubasahra juu ya sarfu ya mtandaoni Jumatatu usiku kupitia mtandao wa kijamii wa X kwenye uzinduzi wa mfumo wa crypto wa wanawe. Anatarajiwa kufanya hivyo kutokea eneo lake la mapumziko la Mar-a-Lago huko Florida.

Rais huyo wa zamani amepangwa kurejea kwenye kampeni siku ya Jumanne atakapohutubia mkutano wa ndani mjini Flint, Michigan pamoja na katibu wake wa zamani wa vyombo vya habari, Gavana wa Arkansas Sarah Huckabee Sanders, na kufuatiwa na mkutano wa kampeni mjini New York kwenye Long Island siku ya Jumatano.

Mwishoni mwa juma, ameratibiwa kuhudhuria na kuhutubia Mkutano wa Kitaifa wa Baraza la Israeli na Marekani mjini Washington, D.C. na Jumamosi atafanya mkutano mjini Wilmington, North Carolina.

Chanzo: Mashirika