1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Harris amkaanga Trump kwenye mdahalo wa runinga

11 Septemba 2024

Mgombea wa urais nchini Marekani wa chama cha Democratic Kamala Harris, alipambana vikali na mshindani wake wa Republican Donald Trump kwenye mdahalo wa televisheni usiku wa kuamkia Jumatano.

https://p.dw.com/p/4kV1w
Uchaguzi Marekani | Trump-Harris wachuana kwenye mdahalo kule Philadelphia
Washindani wakuu wa uchaguzi nchini Marekani mwaka 2024 Donald Trump (Republic) na Kamala Harris (Democratic) wakichuana kwenye mdahalo wa televisheniPicha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Kulingana na utafiti wa maoni ya wapigakura baada ya mdahalo huo, Kamala Harris mwenye umri wa miaka 59 na ambaye pia ni makamu wa rais wa sasa nchini Marekani, alijinadi vyema zaidi na alimpiku Trump katika mdahalo huo wao wa kwanza na pekee, lakini ambao pia ulisheheni vijembe kati yao.

Mdahalo huo uligusia masuala mengi ya kisera ikiwemo uchumi, uhamiaji, usalama na uavyaji mimba. Mdahalo huo umefanyika Philadelphia.

Suala la kwanza kabisa lilikuwa uchumi ambapo Harris alizungumzia historia ya maisha yake ya kukulia ndani ya familia ya kipato cha kati akiwaahidi wapigakura kwamba mpango wake wa uchumi utasaidia familia za aina hiyo. Amesema atazisaidia biashara ndogo na za kati, pamoja na kupunguza kodi kwa familia za kipato cha wastani.

Lakini hoja hizo zilipingwa mara moja na Trump aliyeulaumu utawala wa Rais Joe Biden na Harris kwa kuuharibu uchumi. Trump alisema kiwango cha mfumuko wa bei kwa sasa nchini Marekani kinatisha na kujitapa kwamba alipokuwa madarakani kati ya mwaka 2017 hadi 2021 aliimarisha uchumi wa taifa hilo.

Soma pia: Biden na Harris wafanya kampeni ya pamoja kwa mara ya kwanza

Mitizamo kuhusu uavyaji mimba

Suala jingine lililozusha mjadala mkali ni uavyaji mimba. Kamala Harris ambaye amefanya suala la huduma za afya hasa haki za wanawake kuavya mimba kuwa ajenda muhimu za kampeni yake, alimkosoa Trump kwa msimamo wake kuhusu suala hilo.

"Wamarekani wengi wanaamini katika haki ya mwanamke kufanya maamuzi kuhusu mwili wake. Na ndio maana katika kila jimbo ambalo suala hili limepigiwa kura katika majimbo ya Marekani, watu wa Marekani wamepiga kura ya uhuru,” amesema Harris.

Kwenye majibu yake, Trump amewatuhumu Wademocrat kuwa na kile alichokiita "misimamo laini mno ya kiliberali" akidai baadhi yao wanaunga mkono utoaji mimba hata wakati wa kujifungua.

Soma pia: Uchunguzi waonyesha wapinzani, Harris na Trump wako sambamba kuelekea Ikulu

"Samahani, lazima nijibu, huo ni uongo, nimekuwa mtetezi wa IVF yaani upandikizaji mimba. Unapaswa kuuliza, je utaruhusu uavyaji wa mimba ya miezi tisa, minane au saba? Je utafanya hivyo?” Trump ameuliza.

Hata hivyo, hoja hiyo ilifafanuliwa mara moja na mmoja ya waongozaji mdahalo aliyesema hakuna jimbo nchini Marekani linaloruhusu kuua mtoto akishazaliwa.

Ukabidhiaji wa madaraka

Makabiliano mengine yalishuhudiwa pale swali la Trump kukataa kushindwa na Biden katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kabla ya kujaribu kuyabatilisha matokeo na ikiwa anajutia tukio lolote kuhusu hilo. Trump alijitetea, lakini bila ya kusema waziwazi ikiwa anajutia lolote.

Soma pia: Trump akabiliwa na mashitaka mapya ya kujaribu kuingilia uchaguzi wa 2020

Harris kwa upande wake alisema Trump alifutwa kazi na wapiga kura milioni 81 na kumtaja kuwa kitisho kwa demokrasia.

Trump alimtaja Harris kuwa mgombea dhaifu kuhusu vita vya Gaza huku akisema kuwa anaichukia Israel. Aidha, Trump alijinasibu kuwa na uwezo wa kumaliza vita vya Ukraine na kukomesha wimbi la wahamiaji.

Harris aibuka kidedea, kura za maoni

Kamala Harris na Taylor Swift
Mwimbaji maarufu wa Marekani Taylor Swift (Kulia) amuidhinisha Kamala Harris (Kushoto) kuwa chaguo lake kwa jinsi alivyojinadi kwenye mdahalo wa televisheni na Donald TrumpPicha: AFP

Soma pia: Trump kufanya mkutano wake wa kwanza wa nje tangu jaribio la kumuua

Baada ya mdahalo huo, mwimbaji maarufu wa Marekani Taylor Swift alimuidhinisha Kamala Harris kuwa chaguo lake. Ujumbe wake kwenye ukurasa wake wa Instagram ulipendwa na wafuasi milioni 5.3 kwa saa chache tu.

Kwa upande wa Trump mwenye umri wa miaka 78, alisema huo ulikuwa mjadala wake bora zaidi.

Vyanzo: AFPE, APTN