1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yaondoa hali ya hatari baada ya kutulia kwa vita

Hawa Bihoga
15 Februari 2022

Kura iliopigwa na wabunge kuondoa tangazo hilo la "hali ya hatari" ilitokana na pendekezo la baraza la mawaziri chini ya Abiy Ahmed mwezi uliopita la kupunguza hali ya hatari ambayo ilipaswa kudumu hadi mwezi.

https://p.dw.com/p/4740a
Äthiopien Parlament
Picha: AP Photo/picture alliance

Wabunge 63 kati 312 waliohudhuria kikao hicho walipiga kura ya hapana na 21 walisusia zoezi hilo.Hali ya dharura iliotangazwa mnamo 2 Novemba, baada ya wapiganaji kutoka kundi la Tigray People's Liberation Front (TPLF) kuteka miji miwili muhimu ilio umbali wa kilomita 400 kutoka mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa.

Hatua hiyo ilisababisha watu wengi wa kutoka kabila la Tigray kuzuiliwa huko katika mji mkuu na kwingineko na kuzua shutuma kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu, likiwemo lile la kimataifa la Amnesty International. Hata hivyo bado haijabainika ni lini watu walioshikiliwa chini ya agizo la dharura wataachiliwa.

Soma pia:Marekani yaziondowa Ethiopia, Guinea na Mali kwenye AGOA 

Kutangazwa kwa hali ya dharura kuliambatana na kampeni ya mashambulio ya ndege zisizokuwa na rubani, hatua iliorudisha nyuma wapiganaji wa TPLF kurejea katika mkoa wa  Tigray, kuondoka kwa waasi mwezi Novemba kunaibua matumaini ya kumalizika kwa vita vilivyodumu kwa miezi 15.

Ripoti za mashambulizi ya anga dhidi ya waasi.

Äthiopien | Vereidigung Abiy Ahmed
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

Serikali ya Ethiopia ilitangaza kwamba, haitawafuatilia waasi hao hadi Tigray, lakini katika wiki za hivi karibuni wafanyakazi katika mashirika ya misaada ya kiutu, wameripoti mfululizo wa mashambulizi mabaya ya anga, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani zikilenga eneo hilo ambalo lilikuwa ni uwanja wa vita.

Mwezi uliopita kundi la chama wa ukombozi wa watu wa Tigray- TPLF lilitangaza operesheni ya kijeshi katika eneo jirani la Afar,likisema hatua hiyo ni kujibu mashambulizi ya vikosi vinavyounga mkono serikali ya Ethiopia, hatua inayotajwa  kufifisha matumaini ya kusitishwa kwa mapigani hayo.

Soma pia: Ethiopia yawazuwiya watigray waliofukuzwa Saudi Arabia

Mzozo huo mkubwa umesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na kuwalazimu wengine kuyakimbia makazi yao, huku mamia kwa maelfu wakikabiliwa na njaa, hii ni kwa mujibu wa umoja wa mataifa.

Kwa miezi kadhaa sasa Tigray imekuwa chini ya kile umoja wa mataifa unakiita kuzingirwa. Marekani imeishutumu serikali ya Ethiopia kwa kuzuia misaada ya kiutu, kuwalaumu waasi kwa kukwamisha misaada hiyo.

Himizo la jumuiya ya kimataifa kusitishwa mapigano.

Ujumbe mbalimbali wa kimataifa umekuwa ukihimiza kusitishwa kwa mapigano, ili kutoa nafasi ya ufikishwaji wa misaada ya kiutu katika maeneo yenye mgogoro. Mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Pembe ya Afrika David Satterfield, alitarajiwa kutembelea Ethiopiamapema wiki hii ili kukutana na maafisa wa serikali pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kutoa misaada.

Äthiopien UN-Untergeneralsekretärin Amina Mohammed in Addis Abeba
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Moahammed, aliwambia waandishi mjini Addis Ababa kuwa mazungumzo kati ya serikali ya Ethiopia na viongozi wa Tigray yanaendelea. Lakini serikali ya Ethiopia ilisema hakuna mazungumzo yalioanza bado.Picha: Solomon Muchie/DW

Tigray eneo lenye watu milioni sita, takriban asilimia 40 kati yao wanakabiliwa na "ukosefu mkubwa wa chakula" umoja wa mataifa ulisema mwezi uliopita.

Soma pia: Umoja wa Mataifa kujadili hali ya haki za binadamu Ethiopia

Tathminini isiyo ya kuridhisha iliochapishwa na shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP, ilikuja wakati ambapo mashirika ya kutoa misaada ya kiutu, yakizidi kupunguza kasi ya shughuli zake kutokana na uhaba wa mafuta.

Shirika la afya ulimwenguni WHO, limetoa wito wa "kutokuwa na kizuizi" katika eneo hilo lililokumbwa na vita,likisema kulikuwa na mkwamo katika uwasilishwaji wa vifaa vya matibabu kwa ajili ya kuokoa maisha tangu awamu ya kwanza mnamo mwezi Julai mwaka uliopita, hii ilitokana na ukosefu wa mafuta.

Mapigano makali yalizuka katika mji wa Tigray mwezi Novema 2020, baada ya waziri mkuu Abiy Ahmed kutuma wanajeshi kuiangusha TPLF, chama tawala cha zamani katika eneo hilo, kilisema hatua hiyo ilikuja kutokana na mashambulizi ya waasi katika kambi za jeshi.

Chanzo: AFP