1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la "drone" laua 17 Tigray

Hawa Bihoga
11 Januari 2022

Maafisa wa Tigray wamesema watu 17 wameuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani mkoani Tigray, siku moja baada ya rais wa Marekani Joe Biden kuzungumza kwa simu na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.

https://p.dw.com/p/45OHV
Symbolbild USA Joe Biden am Telefon
Picha: White House/imago images/ZUMA Wire

Rais wa Marekani Joe Biden alipizungumza kwa simu na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alimuelezea wasiwasi wake kuhusiana na kuendelea kwa mashambulizi kama hayo katika vita vinavyoendelea katika eneo hilo.

Utawala wa mkoa huo umesema kwenye ripoti yake kwamba idadi kubwa ya watu waliouawa ni wanawake waliokuwa kwenye mashine ya kusaga unga, karibu na mji wa Mai Tsebri.

Mashambulizi kama hayo ya ndege zisizotumia rubani yamekuwa yakiripotiwa karibu kila siku mkoani Tigray, ambapo shambulio la mwishoni mwa wiki liliilenga kambi ya wikimbizi wa ndani katika mji wa Dedebit ambapo watu 57 waliuawa na wengine zaidi ya 130 walijeruhiwa, wengi wao wakiwa watoto.

Katika mazungumzo ya simu na waziri mkuu Abiy Ahmed, rais wa Marekani Joe Biden alielezea wasiwasi juu ya kamatakamata na mauaji ya raia katika vita dhidi ya vikosi vya Tigray, huku akimsifu Abiy kwa hatua ya kuwaachia wafungwa mashuhuri wa kisiasa.

Serikali ya Ethiopia ilitangaza msamaha wiki iliyopita, kwa baadhi ya wafungwa wa kisiasa, akiwemo kiongozi wa upinzani Jawar Mohammed na maafisa wa juu wa chama cha TPLF.

Äthiopien | Vereidigung Abiy Ahmed
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed bado yuko vitani dhidi ya wanamgambo wa kundi la TPLF katika jimbo la TigrayPicha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

Biden ataka mashambulizi yanayoua raia yakomeshwe

Ikulu ya Marekani, imesema Biden aliibua katika mazungumzo na Abiy, suala la mashambulizi yanayoendelea yanayosababisha vifo vya raia na mateso katika taifa hilo la pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika.

Viongozi hao wawili pia walijadiliana juu ya njia za kuharakisha mazungumzo ya kuleta muafaka wa kusimamisha mapigano, kuboresha ufikishaji misaada kote Ethiopia, na haja ya kushughulikia wasiwasi wa haki za binadamu kwa waethiopia walioathiriwa, ukiwemo wasiwasi kuhusu kukamatwa kwa waethiopia chini ya sheria ya hali ya hatari.

Huko nyuma ukosoaji wa Marekani dhidi ya maafisa wa serikali ya Ethiopia kuhusiana na vita vya wenyewe kwa wenyewe ulisababisha maandamano dhidi ya utawala wa Biden katika taifa hilo la Pembe ya Afrika.

Mazungumzo hayo ya simu yaliombwa na rais Biden, na yalikuja baada ya Jeffrey Feltman, mjumbe maalumu wa Marekani wa kanda ya Pembe ya Afrika anaemaliza muda wake, kuizuru Ethiopia wiki iliyopita kwa ajili ya mazungumzoa na viongozi waandamizi.

Vita vya zaidi ya mwaka mmoja vimesababisha mzozo mbaya wa kibinadamu nchini Ethiopia. Mzozo huo uliingia awamu mpya mwishoni mwa mwezi Desemba, baada ya vikosi vya Tigray kurudi nyuma katika mkoa wao katikati mwa mashambulizi ya kijeshi Tigray, na vikosi vya serikali ya Ethiopia vikasema havitasonga ndani ya mkoa huo.

Soma Zaidi: Umoja wa Mataifa wahofia ghasia zitaisambaratisha Ethiopia

Chanzo: Mashirika