1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Erdogan apata uungwaji mkono wa mpinzani wake

23 Mei 2023

Sinan Ogan ametangaza kumuunga mkono rais Recep Tayyip Erdogan, hatua inayoongeza changamoto dhidi ya mpinzani wake mkubwa Kemal Kilicdaroglu katika duru ya pili ya uchaguzi huo itakayofanyika siku ya Jumapili.

https://p.dw.com/p/4RhQb
Türkei Wahlen Sinan Ogan und Recep Tayyip Erdogan
Picha: Turkish Presidency via AP/AP Photo/picture alliance

Mshindi wa tatu katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais nchini Uturuki Sinan Ogan, ametangaza hatua hiyo jana Jumatatu. 

Mgombea huyo mwenye misimamo mikali ya kizalendo Sinan Ogan, aliyejulikana na wachache kabla ya kampeni alishinda kwa asilimia 5.2 katika duru ya kwanza ya uchaguzi iliyofanyika Jumapili, 14, Mei, amewaambia waandishi wa habari kwamba atamuunga mkono Erdogan katika duru hiyo ya pili ya uchaguzi akisema kampeni zake zimewafanya waturuki wenye misimamo ya kizalendo kuwa muhimu zaidi kwenye siasa za taifa hilo.

Sinan anasema tayari amekutana na wagombea wakuu watakaochuana kwenye duru hiyo ya pili ya tarehe 28 Mei na kujadiliana masuala kadhaa.

"Mimi na wenyeviti wa muungano wetu tulikutana na mgombea wa People's Alliance Recep Tayyip Erdogan, na mgombea wa National Alliance Kemal Kilicdaaroglu, ambao ni wagombea katika duru ya pili ya uchaguzi. Wakati wa mikutano na wagombea wote wawili, tulijadili vipaumbele vyetu vinavyojulikana kwa umma," alisema Ogan

Amesema, muungano wa Kilicdaroglu ulishindwa kuwashawishi juu ya mustakabali wa taifa, na kuongeza kuwa uamuzi wao wa kumuunga mkono Erdogan umezingatia misingi ya harakati zake endelevu za kupambana na ugaidi

Rais Recep Tayyip Erdogan alishinda kwa asilimia 49 katika uchaguzi wa duru ya kwanza. Pembeni yake ni mkewe Ermine Erdogan.
Uchaguzi nchini Uturuki unarudiwa kwa mara ya pili baada ya kukosekana kwa mshindi katika awamu ya kwanzaPicha: ADEM ALTAN/AFP

Erdogan alipata asilimia 49.5 ya kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi, huku Kilicdaroglu akipata asilimia 44.9. Muungano wa chama tawala ulipata wingi wa kutosha bungeni, hatua inayompa Erdogan fursa wakati akipambania awamu ya pili ya urais.

Kwenye mahojiano na shirika la habari la Reuters wiki iliyopita, Ogan alisema lengo lake lilikuwa ni kuviondoa vyama viwili vya Kikurdi kutoka kwenye ulingo wa kisiasa nchini humo pamoja na kuimarisha siasa za kizalendo. Chama kinachounga mkono Wakurdi cha HAP kimemuidhinisha Kilicdaroglu, huku chama cha Huda-Par kikimuunga mkono Erdogan.

Kilicdaroglu aameahidi kubadilisha masuala kadha wa kadha nchini humo kuanzia sera za ndani, za kigeni na hata kiuchumi pamoja na kushughulikia mgogoro wa gharama ya maisha. Erdogan kwa upande wake amesema iwapo watu watampigia kura siku ya Jumapili, watakuwa wamechagua utulivu.

Soma Zaidi:Duru ya pili ya uchaguzi wa urais Uturuki kufanyika Mei 28 

Katika mahojiano na kituo cha utangazaji cha serikali TRT jana usiku, Erdogan amemshukuru Sinan kwa kumuunga mkono akisema anaamini hatua ya kuunganisha nguvu itakuwa na manufaa kwa taifa na kuongeza kuwa yeye na Ogan walikuwa wamekubaliana katika masuala mengi ambayo ni pamoja na vita dhidi ya ugaidi.

Soma Zaidi: Maoni: Erdogan adhihirisha utepetepe wa chunguzi wa maoni