1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS kuwawekea vikwazo watawala wa kijeshi Niger

31 Julai 2023

Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika ya Magharibi (ECOWAS) imetishia kuwawekea vikwazo vikali viongozi wa kijeshi waliopindua serikali ya kiraia na kuingia madarakani kwa nguvu nchini Niger.

https://p.dw.com/p/4UZzu
Nigeria Dringlichkeitssitzung der ECOWAS zum Putsch im Niger
Picha: ECOWAS/Handout via Xinhua/picture alliance

Jumuiya hiyo imetishia pia matumizi ya nguvu ikiwa utaratibu wa kikatiba hautarejeshwa.

Katika kikao cha dharura Jumapili (Julai 30), mataifa ya ECOWAS yalitoa wito wa kuachiwa huru mara moja na kurejeshwa madarakani Rais Mohamed Bazoum, ambaye alikamatwa wakati wa mapinduzi ya Jumatano.

Soma zaidi: Viongozi wa ECOWAS wawaonya viongozi wa mapinduzi, Niger
Vikwazo vyainyemelea Niger

Mataifa hayo yalisema baada ya mkutano wa dharura katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, kuwa ikiwa hali ya kawaida isingerejeshwa ndani ya kipindi cha wiki moja, ECOWAS ingelichukuwa hatua nyengine kali, ikiwemo matumizi ya nguvu na kuwafungulia mashitaka watawala wa kijeshi mjini Niamey.

Aidha shughuli za kibiashara na kifedha kati ya mataifa wanachama wa ECOWAS na Niger zingelisitishwa, na mipaka ya angani na kitaifa kufungwa.

ECOWAS ilisema ingelimteuwa mara moja mjumbe maalum atakayewasilisha masharti hayo kwa watawala wa kijeshi nchini Niger.