1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa kikosi cha EAC nchini DRC ajiuzulu

28 Aprili 2023

Kamanda wa Kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichotumwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jenerali Jeff Nyagah, amejiuzulu.

https://p.dw.com/p/4QfOR
Konflikt im Kongo
Picha: Alexis Huguet/AFP

Taarifa iliyotufikia hivi punde inasema kuwa kujiuzulu kwa jenerali huyo kunakuja siku moja tu baada ya serikali ya Kongo kuitaka Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya marekebisho muhimu kwenye kanuni zinazoongoza operesheni ya kikosi cha Umoja huo mashariki mwa Kongo ili kuepusha kile Kinshasa inachosema ni "hali ya kuchanganya."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo, Christophe Lutundula, aliwaambia waandishi wa habari hapo jana kwamba nchi yake imeionya Jumuiya hiyo kwamba utendaji kazi wa kikosi chake unatia mashaka. Lutundula alikuwa akizungumza mara baada ya mkutano  uliowaleta pamoja wajumbe kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na serikali ya Kongo kutathmini mchakato wa amani wa mashariki mwa nchi hiyo.

Ripoti zinasema Rais  Félix Tshisekedi hakupendezewa na msimamo wa Jenerali Nyagah kukataa kuwaamuru wanajeshi wa kikosi chake kupambana na waasi wa M23, huku mwenyewe akisema ametishiwa mara kadhaa na "mamluki" kutokana na shinikizo la kisiasa.