1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama kipya cha Ujerumani chataka kuisambaratisha Ulaya

Angela Mdungu
16 Januari 2024

Chama kipya cha siasa cha Ujerumani chake Sahra Wagenknecht cha Bündnis Sahra Wagenknecht (BSW), kimesema kinataka kuusambaratisha Umoja wa Ulaya na kuifuta sera ya sasa ya kulinda tabianchi

https://p.dw.com/p/4bJtZ
Chama kipya cha kisiasa nchini Ujerúmani Wagenknecht BSW
wanachama wa Wagenknecht BSW wakiwa mjini Berlin Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Kulingana na rasimu ya chama hicho ya programu ya uchaguzi wa Ulaya, kati ya mipango ya chama cha Wagenknecht ni kuondoa kabisa suala la vyeti vya biashara kikiutaja mfumo huo kuwa usiofaa katika kufikia malengo ya sera ya hali ya hewa. Pia kinatoa wito wa matumizi yasiyo na kikomo ya injini zinazotumia mafuta ya visukuku na kurejeshwa kwa uingizwaji wa mafuta na gesi kutoka Urusi.

Rasimu hiyo imeshuhudiwa na shirika la habari la Ujerumani dpa, na kuripotiwa na gazeti la kila siku la Ujerumani la Frankfurter Allgemeiner. Chama hicho kiliachoanzishwa wiki iliyopita kinakusudia kushiriki kwa mara ya kwanza kwenye uchaguzi wa bunge la Ulaya Juni 9. Rasimu inayoonesha programu hiyo inatazamiwa kujadiliwa katika kongamano la chama cha BSW litakalofanyika Januari 27.

Wagenknecht atangaza rasmi chama chake kipya Ujerumani

Kimsingi mapendekezo hayo yanaukosoa Umoja wa Ulaya kwa mfumo wake wa sasa na inataka usambaratike kwa madai kuwa mfumo huo una athari mbaya kwa Ulaya. Inaeleza kuwa "Kitu kinachoweza kusimamiwa vyema zaidi kwa kufuata demokrasia katika ngazi ya ndani, kikanda na kitaifa hakipaswi kuachwa bila udhibiti wa kundi la wataalamu wa teknolojia wa Umoja wa Ulaya"

Inaongeza pia kuwa, endapo itahitajika, Ujerumani haipaswi kuzingatia sheria za Umoja wa Ulaya. Hatua hii inaweza kuwa mwanzo wa kuachana na msingi wa kanuni za Umoja wa Ulaya zinazofuatwa na nchi wanachama 27. Kanuni hizo hujadiliwa na serikali za mataifa hayo sambamba na bunge la Umoja wa Ulaya.

BSW yasema itazuwia wanachama wapya kujiunga na EU ikiwemo Ukraine

Berlin | Bunge la Ujerumani Bundestag | Dr. Sahra Wagenknecht
Dkt. Sahra Wagenknecht muanzilishi wa chama cha Bündnis Sahra Wagenknecht (BSW) nchini UjerumaniPicha: Jens Krick/Flashpic/picture alliance

Rasimu ya programu ya BSW  inasema pia kuwa, bajeti ya Umoja wa Ulaya haipaswi kuruhusiwa kuongezeka zaidi na kwamba umoja huo hautakiwi kupokea mapato yake. Zaidi ya hapo inabainisha kuwa hakuna ruhusa ya wanachama wapya kujiunga, hata Ukraine. Mapendekezo ya chama cha BSW yanapigia upatu kwa Ulaya kupunguza utegemezi kwa Marekani, yanaongeza kuwa Ulaya inapaswa kuwa mchezaji huru katika uwanja wa kimataifa badala ya kutumiwa katika migogoro ya mataifa makubwa na kuwa kibaraka wa Marekani.

Chama hicho kwenye rasimu yake kinadai kuwa vita vya Ukraine ni vya uwakala kati ya Jumuiya ya kujihami ya NATO  na Urusi na kwamba vinaweza kuwa vilianzishwa kijeshi na Moscow lakini vingeweza kuzuiwa na mataifa ya magharibi na kukoma muda mrefu uliopita.

Zelensky awahimiza viongozi wa EU kuunga mkono mazungumzo ya uanachama wake

Mapendekezo hayo ya programu ya uchaguzi wa Ulaya ya chama hicho pia yanahamasisha kukomesha vita na kufanyika kwa mazungumzo ya amani. Yanabainisha kuwa, ili kuihamasisha Urusi kuingia kwenye majadiliano, hapana budi kusimamisha usafirishaji wowote wa silaha kuingia Ukraine.

Kuhusu sera za uhamiaji, mapendekezo hayo yanatilia mkazo msimamo wa Wagenknetch unaofahamika, yaani, Uhitaji wa michakato ya kuomba hifadhi nje ya mipaka ya Umoja wa Ulaya au kwenye mataifa masikini na kukabiliana na vyanzo vya mapigano. Wagenknetch anakosoa pia kile anachokiona kuwa mtandao wa udhibiti, unaoendeshwa na vyombo vya habari kwa kushirikiana na serikali zinazofanya kazi pamoja.