1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Burundi yafunga mpaka wake na Rwanda

Hawa Bihoga
11 Januari 2024

Burundi imesema imefunga mpaka wake na Rwanda, ikiwa ni wiki mbili sasa baada ya kulituhumu taifa hilo jirani kuwaunga mkono waasi waliofanya mashambulizi nchini humo.

https://p.dw.com/p/4b92t
Picha ya kuunganisha| Marais Evariste Ndayishimiye na Paul Kagame
Rais wa Burundi Eversite Ndayishimiye (kushoto) anashmutumu mwenzake wa Rwanda Paul Kagame kufadhili waasi wa RED-Tabara.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi Martin Niteretse amesema uamuzi huo umeafikiwa baada ya kubaini kuwa, Rwanda inawahifadhi wahalifu wanaowashambulia Warundi.

"Baada ya kubaini kuwa tulikuwa na jirani mbaya, Rais wa Rwanda Paul Kagame tulisitisha mahusiano naye hadi atakapobadilika kuwa bora," aliongeza waziri huyo.

Burundi inasema kundi la RED-Tabara lilifanya shambulizi Desemba 22 karibu na mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuua watu 20, wakiwemo wanawake na watoto.

Soma pia: Ndayishimiye aituhumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa Burundi

Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi tangu wakati huo amekuwa akiinyoshea kidole Kigali akiishtumu kuwaunga mkono waasi hao -- madai ambayo yamekanushwa na serikali ya Rwanda.

Uhusiano kati ya Burundi na Rwanda mara nyingi umekuwa na pandashuka chungumzima, ingawa ulianza kuimarika baada ya Ndayishimiye kuchukua madaraka mwaka wa 2020, lakini umedorora tena kutokana na ushiriki wa Burundi katika kampeni za usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Kundi la RED-Tabara linashtumiwa kuendesha mashambulizi makali  katika taifa hilo la Afrika Mashariki.Tangu 2015 kundi hilo halikuwa likifanya mashambulizi lakini tangu Septemba 2021, limekuwa likifanya mashambulizi kadhaa, ikiwa ni pamoja na dhidi ya uwanja wa ndege wa jiji kuu la Bujumbura.