1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Biden awasili Uingereza kabla ya mkutano wa NATO

10 Julai 2023

Rais wa Marekani Joe Biden amewasili Uingereza jana na atakutana hii leo na Waziri Mkuu Rishi Sunak na Mfalme Charles III kabla ya kuelekea nchini Lithuania kuhudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya kujihami ya NATO.

https://p.dw.com/p/4TeCQ
Marekani Joe Biden Uingereza
Rais wa Marekani Joe Biden akiwasili UingerezaPicha: Kin Cheung/dpa/picture alliance

Biden anatarajiwa kuyatembelea mataifa matatu ya Ulaya katika ziara yake. Nayo ni Uingereza, Lithuania na Finland ambayo imejiunga hivi karibuni na Jumuiya ya kujihami NATO.

Kabla ya kuwasili mjini London hapo jana, Ikulu ya White House ilisema ziara ya Biden inajaribu kuimarisha uhusiano wa karibu na Uingereza, huku Biden mwenyewe akisema Marekani haina mshirika wa karibu kuliko Uingereza.

Biden atakutana na waziri mkuu Rishi Sunak ambaye wanatarajia kuzungumzia mkutano ujao wa kilele wa NATO na vita vya Ukraine, na baadaye rais huyo wa Marekani atakutana na Mfalme Charles III katika kasri la Windsor, na kujadili masuala ya mazingira. 

Baadaye leo usiku, Biden ataelekea katika mji wa Vilnius nchini Lithuania  kuhudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami NATO utakaoanza siku ya Jumanne na unaolenga kuonesha mshikamano kwa Ukraine katika mapambano yake dhidi ya uvamizi wa Urusi.

USA Washington | Pressekonferenz: Joe Biden zu Krankenversicherung
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Samuel Corum/abaca/picture alliance

Katika mahojiano na kituo cha habari cha CNN, Biden amesema Kyiv haijawa tayari kujiunga na muungano huo wa kijeshi huku akionya kuwa kuijumuisha Ukraine wakati huu mzozo ukiendelea, kunaweza kuiingiza NATO kwenye vita vya moja kwa moja na Urusi. Amesisitiza kuwa itachukua muda hadi Kyiv kuweza kujiunga na NATO.

Soma pia: Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg aahidi msaada zaidi kwa jeshi la Ukraine

Naye Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema anatarajia matokeo bora zaidi katika mkutano huo wa kilele na kusema kuwa mwaliko wa Ukraine kujiunga na NATO ungelituma ujumbe kwamba muungano huo hauiogopi Urusi.

Hata hivyo Biden ameihakikishia Ukraine kuwa Washington inaweza kuipatia Kyiv msaada kama unaotolewa kwa Israel hadi itakapojiunga na muungano huo wa kijeshi.

Mkutano wa NATO kujadili uanachama wa Sweden

Mkutano huo wa NATO wa siku mbili unatarajia pia kujadili ombi la Sweden la kujiunga na muungano huo , ambalo hadi sasa limezuiliwa na Uturuki. Mshauri Mkuu wa Usalama wa Ikulu ya White House Jake Sullivan amesema Rais Joe Biden amefanya mazungumzo na mwenzake wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan juu ya suala hilo na mengineyo:

" Tulipokuwa kwenye ndege, Rais Biden alipata fursa ya kuzungumza na Rais Erdogan wa Uturuki. Walizungumza kuhusu masuala kadhaa kuhusiana na mkutano ujao na hata vita vya Ukraine. Na pia uungwaji mkono thabiti wa Uturuki, hasa katika msaada wa kijeshi kwa mahitaji ya ulinzi ya Ukraine. Pia walizungumza kuhusu uanachama wa Sweden na walikubaliana kwamba watakuwa na fursa ya kuketi pamoja huko Vilnius."

Deutschland Schweden Premierminister Ulf Kristersson Olaf Scholz
Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson Picha: ANNEGRET HILSE/REUTERS

Aidha, Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson  atakutana hii leo na Rais Erdogan  katika jaribio la kumaliza mzozo wa kidiplomasia juu ya kukwama kwa mpango wake wa uanachama wa NATO.

Soma pia: Sweden na Uturuki zakutana Brussels kuhusu NATO

Erdogan alimueleza Biden kuwa Sweden imechukua hatua kadhaa katika mwelekeo sahihi unaoweza kupelekea Uturuki kuunga mkono ombi la Stockholm kujiunga na NATO lakini akasema kuwa hatua hizo hazikuwa na manufaa kwa kwani wafuasi wa PKK waliendelea kufanya maandamano nchini Sweden.

Katika suala jingine, Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol ambaye anatarajiwa pia kuhudhuria mkutano huo wa NATO ili kutafuta ushirikiano zaidi wa kimataifa, amesema ni wakati wa Jumuiya ya kimataifa kuonesha kuwa azma yao ina nguvu za kuizuia Korea Kaskazini kutengeneza silaha za nyuklia.