1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUswisi

Erdogan apuuza shinikizo la kuruhusu Sweden kujiunga na NATO

14 Juni 2023

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amepuuzia mashinikizo ya kimataifa yanayoongezeka kwa Ankara ya kuridhia ombi la Sweden kujiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO kabla ya muungano huo wa ulinzi kukutana mwezi Julai.

https://p.dw.com/p/4SZCl
Türkei | Recep Tayyip Erdogan
Picha: Aytac Unal/AA/picture alliance

Maafisa wa mataifa ya magharibi walitaraji kwamba rais Recep Tayyip Erdogan atalegeza msimamo wake juu ya suala hilo, na hasa baada ya kurejea mamlakani katika uchaguzi wa marudio wa mwezi uliopita. 

Erdogan aliashiria kupuuzilia mbali kishindo kutoka kwa washirika wake wa NATO, kufuatia matamshi yaliyochapishwa na ofisi yake kabla ya maafisa wa Uturuki na Sweden, Finland na NATO kukutana kwa ajili ya mazungumzo hii leo ya namna ya kukabiliana na pingamizi la Ankara linaloizuia Sweden kujiunga na muungano huo. Erdogan alinukuliwa akisema Sweden ina matarajio, lakini haimaanishi kwamba watakubaliana nayo. Akaongeza ili wote waweze kuyafikia matarajio hayo, kwanza Sweden inatakiwa itimize wajibu wake. 

Uturuki inaituhumu Sweden kwa kuwahifadhi wanachama wa kundi la wanamgambo wa Kikurdi, ambao Uturuki inasema ni magaidi na waliohusika kwenye jaribio la mapinduzi la mwaka 2016. Msururu wa maandamano mjini Stockholm ambayo ni pamoja yale yaliyofanywa na mwanaharakati wa kupinga Uislamu aliyechoma kitabu cha Quran nje ya ubalozi wa Uturuki pia yalichochea mvutano. 

Erdogan amewaambia waandishi wa habari akiwa kwenye ndege akirejea nyumbani kutoka Arzebaijan kwamba Sweden isitarajie mabadiliko ya msimamo wa Uturuki hadi pale itakapochukua hatua ya kuzuia maandamano ya kuipinga Uturuki huko mjini Stockholm na kuongeza kuwa Uturuki haiwezi kuridhia ombi hilo la Sweden.

Uturuki inaitaka Sweden kutimiza wajibu wake na kusuluhisha mvutano uliopo kati ya mataifa hayo ili kufikia muafaka wa suala la nchi hiyo kujiunga na NATO
Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Istanbul baada ya mazungumzo na rais Recep Tayyip Erdogan.Picha: Islam Yakut/AA/picture alliance

Taarifa zilisema rais Joe Biden wa Marekani alimuongezea shinikizo Erdogan wakati walipozungumza kwa simu siku moja kabla kiongozi huyo wa Uturuki hajaongeza muhula mwingine utakaodumu hadi 2028. Na kama haitoshi, hapo jana, msemaji wa ikulu ya White House Karine Jean-Pierre aliwaambia waandishi wa habari mjini Washington kwamba Sweden itakuwa mwanachama wa NATO hivi karibuni, akisema ni mshirika imara na mwenye uwezo kiulinzi ambaye anaweza kuchangai pakubwa katika usalama wa Ulaya.

Amesema "Sweden ni mshirika imara na thabiti. Kwa hiyo tunaamini na mmeshasikia kutoka kwa rais huyu mara kadhaa kwamba tunaamini Sweden inatakiwa kuwa mwanachama wa NATO haraka iwezekanavyo. Hiki ndicho rais amesema. Anakiunga mkono. Na ndicho tulichokiona bungeni pia."

Sweden na Finland walipeleka maombi ya uanachama kwa pamoja, baada ya Urusi kuivamia Ukraine mwaka jana. Finland ilikubaliwa uanachama Aprili 31 baada ya bunge la Uturuki kuidhinisha ombi lake, lakini ikakataa kuiidhinisha Sweden. 

Nia ya NATO ni kuijumuisha Sweden kwenye muungano huo katika mkutano wake wa kilele utakaofanyika Lithuania Julai 11-12.  Hata hivyo Sweden imesema katika taarifa ya hivi punde kwamba mazungumzo na Uturuki yataendelea, bila kutoa taarehe maalumu.

Soma zaidi: Finland yatumai kukubaliana na Uturuki kuhusu NATO