1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUswidi

Sweden na Uturuki zakutana Brussels kuhusu NATO

6 Julai 2023

Maafisa waandamizi wa Sweden na Uturuki watakutana Alhamis katika makao makuu ya NATO mjini Brussels, ili kuangazia hatua za Uturuki kuipinga Sweden kujiunga na muungano huo wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/4TUme
NATO Headquarter Brüssel
Makao Makuu ya NATO mjini BrusselsPicha: Geert Vanden Wijngaert/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Mkutano huo pia utatazama iwapo kuna lolote linaloweza kufanyika kwa ajili ya kupatikana mwafaka.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg atauongoza mkutano huo ambao utawaleta pamoja mawaziri wa mambo ya nje, wakuu wa ujasusi na washauri wa kitaifa wa usalama wa nchi husika.

Maafisa waandamizi wa Finland ambayo ilijiunga na NATO mwezi Aprili baada ya kuridhia kuyatimiza matakwa ya Uturuki, itashiriki mazungumzo hayo pia.

Schwedens Ministerpräsident Kristersson / Joe Biden
Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson(kushoto) na Rais wa Marekani Joe Biden(kulia)Picha: Evan Vucci/AP/dpa/picture alliance/dpa

Uturuki yasema Sweden haijatimiza masharti yake kikamilifu

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan amesema wataziangazia hatua zilizochukuliwa na Sweden na Finland hasa katika muktadha wa kupambana na ugaidi, tangu ulipofanyika mkutano wa mwisho baina yao mnamo Juni 14 huko Ankara, Uturuki.

Ni Uturuki na Hungary tu ndizo vigingi vya Sweden kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo. Wanachama wengine 29 wamesema kwamba Sweden imechukua hatua za kutosha kuyatimiza masharti ya Uturuki. Sweden imekubali kubadili sheria zake dhidi ya ugaidi na imeondoa marufuku ya silaha kwa Uturuki, miongoni mwa mambo mengine mengi.

Ila Uturuki inaituhumu Sweden kwa kuyapendelea sana makundi ambayo Uturuki inayaona kama kitisho kwa usalama wake. Miongoni mwa makundi hayo ni makundi ya wanamgambo ya Kikurdi na watu waliohusishwa na jaribio la mapinduzi la mwaka 2016 nchini Uturuki.

Biden kuwasiliana na marais wa Uturuki na Hungary?

Hapo Jumatano Rais wa Marekani Joe Biden alimkaribisha katika Ikulu ya White House Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson, kama njia ya kuonyesha mshikamano kuelekea mkutano wa kilele wa NATO.

Türkei | Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Reccep Tayyip ErdoganPicha: Aytac Unal/AA/picture alliance

"Lakini tuko tayari kwa mkutano wa kilele wa NATO wiki ijayo. Na nataka kusisitiza tena, Marekani inaunga mkono kikamilifu uanachama wa Sweden katika NATO. Ni rahisi kabisa, Sweden itaiongezea nguvu jumuiya yetu na ina thamani sawa kama ile tuliyo nayo kwenye NATO. Ninasubiri kwa hamu sana uanachama wenu," alisema Biden.

Msemaji wa Ikulu ya White House Karine Jean-Pierre hakusema iwapo Biden anapanga kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na marais wa Uturuki na Hungary kuhusiana na suala hilo kabla ya mkutano wa kilele.

Hungary pia haijaridhia hatua ya Sweden kutaka kujiunga na jumuiya ya NATO ila haijaweka bayana mashaka yake. Maafisa wa NATO wanatazamia Hungary ifuate mkumbo mara tu Uturuki itakapoiondolea Sweden pingamizi.

Kupanuliwa kwa Jumuiya ya NATO kunahitaji idhini ya wanachama wote 31 walioko sasa.

Mwandishi: Jacob Safari/AFP/Reuters

Mhariri: Babu Abdalla