1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kujadili Ukraine kwa dharura

28 Februari 2022

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana limechukua hatua ya nadra ya kuitisha mkutano wa dharura wa wanachama wote 193 wa Baraza Kuu la Umoja huo kujadili kuhusu azimio la kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/47hCs
BdTD | Slowakei
Picha: Peter Lazar/AFP/Getty Images

Baada ya Urusi kutumia kura yake ya turufu kuzuia azimio hilo kwenye baraza la usalama wiki iliyopita, sasa mataifa ya magharibi wana matumaini ya idadi kubwa ya wanachama kulaani uvamizi huo wa Urusi kwenye mkutano huo uliopangwa kuanza kufanyika baadae leo.

Soma Zaidi: Rais Zelensky aulilia Ulimwengu 

Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Barbara Woodward amesema Urusi haiwezi kuuzuia ulimwengu kuungana pamoja kulaani uvamizi huo.

Soma Zaidi: Rais wa Ukraine atoa agizo kwa wananchi wote kufanya maandalizi ya kujihami

Mkutano huu utakuwa wa 11 wa dharura wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka 70 tangu kuanzishwa kwake.

Kwa kuwa mataifa mengi yanatarajiwa kutoa hotuba, mkutano huo huenda ukadumu kwa siku saba.

Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja huo Nicola De Riviere alitangaza kwamba baraza la usalama litafanya mkutano hii leo kuhusiana na athari za kibinaadamu kufuatia uvamizi huo, kikao kilichoombwa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ili kuhakikisha ufikishwaji wa misaada kwa idadi inayoongezeka ya wale wenye mahitaji nchini Ukraine.

Mikutano hiyo yote inafuatia kura ya turufu ya Urusi kwenye azimio la baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaliyomtaka Urusi kusimamisha mara moja shambulizi nchini Ukraine na kuondoa wanajeshi wake wote. Matokeo ya kura hiyo yalikuwa ni 11-1. China, India na Umoja wa Falme za Kiarabu hawakupiga kura hiyo.