1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani yupo nchini Mali.

Zainab Aziz Mhariri: Bruce Amani
12 Aprili 2022

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amewatembelea wanajeshi wa Ujerumani katika kambi ya Castor iliyopo Gao kaskazini mwa Mali. Ujerumani itaamua juu ya kuongezwa muda wa jeshi lake nchini Mali.

https://p.dw.com/p/49qS7
Mali | Besuch Aussenministerin Annalena Baerbock
Picha: Florian Gaertner/photothek/picture alliance

Waziri wa Mambo Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameitembelea kambi ya Castor, ambapo sehemu kubwa ya wanajeshi wa Ujerumani wapatao 1,100  ni miongoni mwa vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani (MINUSMA). Mbali na wanajeshi wa Ujerumani kushiriki katika kikosi hicho cha MINUSMA, takriban wanajeshi wengine 320 wanashiriki katika mpango wa kutoa mafunzo ya kijeshi unaoendeshwa na Umoja wa Ulaya, EUTM.

Soma pia: Waziri wa ulinzi wa Ujerumani awapa moyo wanajeshi Mali

Kulingana na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock atafanya mazungumzo leo hii na kiongozi wa kijeshi, Assimi Goita, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali Abdoulaye Diop halafu ataendelea na safari yake kuelekea nchini Niger kwa mazungumzo na Rais Mohamed Bazoum na Waziri wa Mambo ya Nje Ibrahim Yacoubou.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock akiwa ndani ya ndege ya kijeshi akitokea Bamako kulelekea Gao nchini Mali.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock akiwa ndani ya ndege ya kijeshi akitokea Bamako kulelekea Gao nchini Mali.Picha: picture alliance/dpa

Waziri Baerbock akitokea katika mji mkuu wa Mali, Bamako kuelekea katika mji wa Gao hakusafiri kwa ndege rasmi kama ilivyo kawaida bali aliruka kwa ndege ya kijeshi hii ikielezwa kuwa ni kutokana na sababu za kiusalama.

Soma pia:Hatma ya vikosi vya Ufaransa Mali mashakani

Mkuu wa Umoja wa Ulaya anayesimamia sera ya Mambo ya Nje, Josep Borrell, amesema, baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Ulaya, Umoja wa Ulaya utasimamisha majukumu yake yote ya kutoa mafunzo nchini Mali lakini utaendelea kuwepo katika eneo la Sahel.

Mkuu wa Umoja wa Ulaya anayesimamia sera ya Mambo ya Nje, Josep Borrell.
Mkuu wa Umoja wa Ulaya anayesimamia sera ya Mambo ya Nje, Josep Borrell.Picha: Alexey Vitvitsky/Sputnik/picture alliance

Borrel amesema matukio yanawalazimisha kufanya maamuzi haya kutokana na kwamba hakuna hakikisho la kutosha la usalama kutoka kwa serikali ya mpito ya Mali juu ya kuingiliwa kati na kundi la Wagner kutoka Urusi.

Urusi imekanusha kuhusika na makosa yoyote nchini Mali au katika nchi nyingine yoyote ambako kundi la Wagner linaendesha shughuli zake. Rais Vladmir Putin amesema wakandarasi hao wana haki ya kufanya kazi popote pale duniani mradi tu hawavunji sheria. Mali na Urusi hapo awali zilisema kuwa kundi la Wagner halijumuishi mamluki bali wakufunzi wanaowasaidia wanajeshi wa ndani kutumia vyema vifaa vilivyonunuliwa kutoka Urusi.

Soma:Umoja wa Mataifa wataka kuchunguza mauwaji ya Mali

Waziri Baerbock alibainisha kabla ya kuanza safari yake hapo jana Jumatatu jioni kwamba serikali ya Mali imevuruga imani ya jamii ya kimataifa katika miezi ya hivi karibuni, hasa kwa kuing'oa serikali ya mpito ya kidemokrasia na kisha kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na Urusi ikiwa ni pamoja na uwepo wa mamluki na hatua za polepole za mabadiliko kuelekea demokrasia nchini Mali.

Jeshi la Ujerumani litakamilisha majukumu yake nchini Mali ifikapo Mei 31 hivyo basi serikali ya Ujerumani inajiandaa kuamua iwapo muda wa jeshi lake nchini Mali utaongezwa au la. Bunge litapaswa kutoa maamuzi juu ya mustakabali wa jeshi la Ujerumani nchini Mali.    

Vyanzo:DPA/RTRE/AFP