1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Senegal yaitaka Ujerumani kubakisha majeshi yake Mali

22 Februari 2022

Rais wa Senegal, Macky Sall ameitaka Ujerumani kuyabakisha majeshi yake Mali, huku kukiwa na hali ya sintofahamu kuhusu mustakabali wa nchi hiyo baada ya Ufaransa kutangaza kuwaondoa wanajeshi wake.

https://p.dw.com/p/47OwS
Bundespräsident Steinmeier im Senegal | Präsident Macky Sall
Picha: SEYLLOU/AFP

Sall ameutoa wito huo jana katika mkutano na waandishi habari kwenye mji mkuu wa Senegal, Dakar pamoja na Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, ambaye anaizuru nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Idadi ya wanajeshi wa Ujerumani MINUSMA na EUTM

Ujerumani ina wanajeshi 1,170 kama sehemu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA. Ujerumani pia imechangia wanajeshi 328 kama ujumbe wa Umoja wa Ulaya wa kutoa mafunzo nchini Mali, EUTM.

Lakini Ufaransa wiki iliyopita ilitangaza kuwaondoa maelfu ya wanajeshi wake Mali, iliyoko kwenye ukanda wa Sahel inayokabiliwa na mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi, hatua iliyosababisha mashaka kuhusu mustakabali wa ushiriki wa jeshi la Ujerumani.

Mali Bundeswehr in Gao
Mwanajeshi wa Ujerumani ambaye ni sehemu ya kikosi cha MINUSMAPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Sall ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, amesema wanavihitaji vikosi vya Ulaya, MINUSMA na Ujerumani nchini Mali. Kwa upande wake Rais Steinmeier amesema Ujerumani inapaswa kubakia katika hali ambayo inachangia uthabiti katika ukanda wa Sahel.

Steinmeier amefafanua kuwa uamuzi wa mwisho utalitegemea bunge la Ujerumani, ambalo linatarajiwa kuamua iwapo waongeze muda wa ushiriki wa nchi hiyo katika kikosi cha MINUSMA na EUTM nchini Mali ifikapo mwezi Mei. Hata hivyo, rais huyo wa Ujerumani aliyeko kwenye ziara ya siku tatu nchini Senegal ametoa wito wa ushirikiano imara zaidi kati ya Ulaya na Senegal.

Ujerumani kuzingatia usalama wa wanajeshi

"Majadiliano tunayoyafanya nchini Ujerumani kuhusu hali ya Mali na mustakabali wa ushiriki wa Ujerumani katika MINUSMA, yanaendeshwa kwa umakini na uwajibikaji, tukizingatia kwamba ni kwa faida yetu mzigo haupaswi kuwa mkubwa tena kwa nchi kama vile Senegal, lakini pia tunapaswa kujadiliana hilo kwa kuzingatia usalama wa wanajeshi wa Ujerumani," alisema Steinmeier.

Steinmeier amesema kutokana na tofauti zilizopo ni lazima watafute njia ya ushirikiano wa karibu wenye tija. Akiitaja Senegal kama nchi yenye demokrasia imara na kinara wa utulivu katika ukanda wa Sahel, Steinmeier amesema nchi hiyo imekuwa na jukumu muhimu sana.

Brüssel | Christine Lambrecht, Bundesministerin der Verteidigung
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Christine LambrechtPicha: Martin Luy/DW

Aidha, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Christine Lambrecht amesema ana mashaka kuhusu kuendelea kushiriki katika ujumbe wa kutoa mafunzo wa Umoja wa Ulaya na amehoji iwapo Ujerumani inapaswa kuendelea kujitolea MINUSMA bila msaada wa Ufaransa.

Viongozi hao wawili pia wamezungumzia utengenezaji wa chanjo ya virusi vya corona barani Afrika. Rais Sall amesema Afrika inataka kutengeneza chanjo zake yenyewe badala ya kupatiwa kama msaada. Steinmeier amesema anaamini takribani asilimia 100 ya chanjo za COVID-19 zinatengenezwa nje ya Afrika.

Marais hao wa Ujerumani na Senegal pia wamejadiliana kuhusu masuala ya uchumi na biashara.

Huku hayo yakijiri, kiongozi wa kijeshi wa Chad, Mahamat Idriss Deby Itno ametangaza kuwa nchi yake itaongeza majeshi katika kikosi cha MINUSMA baada ya Ufaransa kujiondoa. Luteni Jenerali Mahamat amesema Mali ni kitovu cha ugaidi katika ukanda wa Sahel.

(AFP, DPA)