1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

25 Januari 2019

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeshuhudia tukio la kihistoria baada ya kiongozi wa  upinzani Felix Tshisekedi kuapishwa rasmi hapo Alhamisi kuanza kuwatumikia wananchi wa Kongo.

https://p.dw.com/p/3CC8G
Kongo Felix Tshisekedi
Picha: picture-alliance/dpa/B. Curtis

die tageszeitung 

Tshisekedi amepata urais kutokana na hisani ya rais wa hapo awali Joseph Kabila. Tshisekedi  ambae ni mtoto wa Etienne Tshisekedi aliyekuwa mpinzani shupavu dhidi ya tawala za Mobutu na  za Kabila baba na mtoto, ameingia madarakani kwa ushindi wa mashaka. Gazeti hilo linasema waangalizi wa uchaguzi karibu wote walikuwa na uhakika kwamba mshindi wa kweli wa uchaguzi alikuwa mgombea mwingine wa upinzani, Martin Fayulu na linaeleza zaidi kwamba tume ya uchaguzi pamoja na mahakama ya katiba ziliamua kumpa ushindi Felix Tshisekedi  anayeingia madarakani akiwa amebeba mzigo mkubwa wa jina la baba yake lakini, bila ya kuwa na sifa za baba yake Etienne Tshisekedi.

Mnamo mwaka 2017 mwanasiasa huyo aliitisha maandamano, lakini yeye mwenyewe alisafiri kwenda Addis Ababa. Mnamo mwezi Novemba aliitisha maandamano mengine lakini alikaa nyumbani kwake hadi polisi walipokuja kuizingira nyumba yake. Gazeti la die tageszeitung linasema mara kadhaa aliwaacha wafuasi wake solemba, jee safari hii atafanya hivyo tena kwa kuukumbatia upande wa serikali inayoondoka madarakani?

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema katika makala yake ya wiki hii kwamba tangu kutiwa saini mkataba wa amani nchini Sudan Kusini hali imekuwa shwari. Jee hali hiyo itawawezesha wakimbizi wa nchi hiyo kurejea nyumbani. Gazeti hilo linatuelezea mkasa wa mkimbizi mmoja kutoka Sudan Kusini aliyekimbilia Uganda, bi Roy Rubin mwenye umri wa miaka 50: 

Mama huyo amesema, sasa nyumbani kuna amani lakini hana uhakika iwapo anaweza kurejea. Miaka mitano iliyopita mama huyo Roy Rubin alikimbilia Uganda pamoja na watoto wake wawili. Miezi miwili iliyopita kaka yake alipakia masanduku yake na kwenda nyumbani, Sudan Kusini kuona jinsi hali ilivyo halafu arudi tena Uganda kuichukua familia yake. Roy Rubin amesema kaka yake hakurudi tena Uganda, aliuliwa!

Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba mkataba wa amani ulitiwa saini mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka uliopita baina ya serikali na waasi nchini Sudan Kusini. Iwapo amani itadumu kutokana na mkataba huo, mkimbizi huyo anayeishi Uganda kwa sasa, mama Roy Rubin hana ukahika.Mama huyo si mtu wa pekee asiyekuwa na imani na ahadi zinazotolewa na wanasiasa.

Neue Zürcher

Watu nchini Zimbabwe wamejitokeza barabarani kuandamana ili, kupinga uamuzi wa  serikali wa kupandisha bei ya petroli. Polisi walitumia mabavu kuwakabili waandamanaji hao na tume ya haki za binadamu imesema wanajeshi na polisi waliwafanyia wananchi ukatili mtindommoja. Gazeti la Neue Zürcher linasema majeshi ya usalama yanadai kwamba ukatili huo ulifanywa na watu walioiba sare za jeshi na kuzivaa na kujifanya wanajeshi na polisi!

Gazeti hilo linasema rais Emmerson Mnangagwa ameagiza kufanyika uchunguzi na limemkariri rais huyo akisema kwenye Twitter, endapo itabidi, waliohusika watatimuliwa kazini lakini gazeti hilo pia linakumbusha. Baada ya uchaguzi wa mwaka uliopita rais Mnangagwa alitoa ahadi kama hiyo, wanajeshi walipotenda ukatili lakini rais huyo hakuchukua hatua yoyote .

die  tageszeitung 

Mwanaharakati maarufu Oby Ezekwesili ameliondoa jina lake kutoka kwenye orodha ya wagombea urais katika uchaguzi utakaofanyika mwezi ujao nchini Nigeria. Mama huyo anajulikana duniani kote kama mwanzilishi mwenza wa shirika la kupambana na rushwa duniani, pamoja na kampeni ya kuwakomboa wasichana waliotekwa nyara na magaidi wa Boko Haram, maarufu #BringBackOurGirls.

Gazeti la die tageszitung limemnukulu Ezekwesili akisema amefanya umauzi huo baada ya kushauriana kwa undani na watu wa ndani na nje ya Nigeria lakini gazeti hilo pia linatilia maanani kwamba tangu mwezi Oktoba mwaka jana, hadi sasa, fedha alizochangisha kwa ajili ya kampeni hajizafikia hata dola 7,000 na kiwango kinachohitajika ni kuanzia dola 15,000.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Iddi Ssessanga