1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

11 Januari 2019

Yaliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na maoni ya wahariri baada ya tume ya uchaguzi nchini Kongo CENI kumtangaza kiongozi wa upinzani Felix Tshisekedi kuwa mshindi.

https://p.dw.com/p/3BMKm
Kongo, Kinshasa: Nach den Wahlen im Kongo - Félix Tshisekedi
Picha: picture-alliance/dpa/J. Delay

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linasema katika  maoni yakelinasema kutangazwa kwa kiongozi  wa upinzani Tshisekedi kuwa mshindi wa  uchaguzi maana yake ni kushuhudia mabadiliko ya uongozi yaliyofanyika kwa njia  ya kidemokrasia.

Gazeti hilo limeandika: Itakuwa fursa ya kihistoria, ya kulipeleka bara la Afrika mbele endapo Felix Tshisekedi  kweli atakuwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Yumkini ingeliwezekana kwa Kongo kuondokana na kizungumkuti cha migogoro na umwagikaji damu hali ambayo imeiandama nchi  hiyo yenye karibu watu miloni 90 kwa muda wa miaka mingi.

Inaaminika kwamba ushindi wa Tshisekedi ni wa udanganyifu. Kulingana na kile kinachoaminiwa na watu wengi nchini Kongo  mshindi wa kweli ni kiongozi mwengine wa  upinzani Martin Fayulu na zipo hoja zenye mashiko juu ya madai  hayo.  Gazeti la die tageszeitung linasema Fayulu ni mgombea aliyekuwa anawakilisha maslahi ya wapinzani wa Joseph Kabila wanaoishi nje ya nchi.  

Neue Zürcher  

 Nchini Gabon gazeti la Neue Zücher limeandika juu ya jaribio la kuiangusha serikali lililofanywa na wanajeshi waasi na linatuambia kwamba kikundi cha askari kilijaribu kutwaa mamlaka nchini humo kwa kusoma tamko kwenye kituo cha radio ya taifa, la kuwataka wanajeshi na wananchi kwa  jumla wajiunge na njama za askari hao za kuiangusha serikali. Askari hao walipanga njama zao wakati rais Ali Bongo akiwa nje kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya maradhi ya kiharusi yaliyompata wakati akiwa nchini Saudi Arabia. Hata hivyo gazeti hilo la Neue Zücher linatilia maanani kwamba jaribio la askari hao liligunduliwa na kuzimwa.

Askari wawili waasi waliuliwa na wengine watatu walikamatwa. Gazeti la Neue Zücher linatueleza mambo yanayoweza kusababisha hatua iliyochukuliwa na askari hao waasi. Kwa baadhi ya watu, nchini Gabon, Ali  Bongo si mzaliwa wa nchi hiyo. Yeye ana asili ya  Nigeria. Alichukuliwa kutoka Nigeria wakati wa  vita vya Biafra na kulelewa nchini Gabon na kwa  hivyo kama mgeni hastahili kuwa mkuu wa nchi. Suala hilo linaendelea kuzingatiwa na mahakama  mbalimbali za nchini Gabon na Ufaransa. Gazeti hilo la Neue Zücher pia linasema ukoo wa Bongo umetawala Gabon kwa muda wa miaka mingi na umelimbikiza kiasi kikubwa sana cha mali wakati thuluthi moja ya wananchi wanaishi katika umasikini.

Naam msikilizaji sasa tunaigeukia Sudan ambako rais wa nchi hiyo Omar al-Bashir  anapanda jukwaani na kunengua wakati  maandamano makubwa ya kumpinga yanazidi kupamba moto. Gazeti la Süddeutsche linatueleza  zaidi:

NARR: Kwa muda wa wiki kadhaa sasa, maalfu ya  watu nchini Sudan wamekuwa wanafanya  maandamano ya kumpinga rais Omar al-Bashir  alieingia madarakani kwa mabavu tangu mwaka 1989. Katika kila pembe ya nchi watu wanajitokeza kumpinga al -Bashir. Hii si mara ya kwanza kwa rais huyo kupingwa na maaflu ya  watu barabarani lakini wakati wote alikuwa na  majawabu. Aliwatia ndani wapinzani, aliwanunua na kuwashirikisha katika serikali yake na mara  nyingine alipunguza bei ya mahitaji muhimu ili  kuwaliwaza wananchi.

Süddeutsche Zeitung

Gazeti hilo linasema safari  hii watu wanaompinga al -Bashir ni wengi sana. Sasa hana njia nyingine ila kupanda jukwaani na kuyatikisia mbali matatizo kwa kunengua. Gazeti la Süddeutsche linatueleza chanzo cha matatizo hayo kwamba ghasia za hivi karibuni zilianza mwishoni  wa mwezi Novemba baada ya serikali kupunguza ruzuku kwa ajili ya kufidia bei za unga wa ngano na mafuta ya petroli.

Uamuzi huo ulisababisha kuongezeka kwa bei ya mkate mara nne lakini uamuzi wa serikali wa kupunguza ruzuku ulitokana na masharti ya shirika la fedha la  kimataifa IMF ili Sudan ipatiwe mkopo na shirika hilo. Serikali ya al- Bashir imepungukiwa  fedha. Tangu kujitenga kwa Sudan Kusini, serikali ya al-Bashir imepoteza nusu ya mapato yaliyotokana na mauzo ya mafuta yaliyoko Sudan Kusini.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef