1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Merkel Algeria yamalizika.

Kitojo, Sekione17 Julai 2008

Kansela wa Ujerumani ameangalia zaidi maslahi ya kibiashara katika ziara yake ya siku mbili nchini Algeria.

https://p.dw.com/p/EeFL
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akipokewa uwanja wa ndege wa mjini Algiers na mwenyeji wake rais Abdelaziz Bouteflika jana Jumatano wakati alipoanza ziara yake ya siku mbili ambayo imemalizika leo Alhamis.Picha: AP


►◄




Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameweka maslahi ya kibiashara mbele kabisa wakati wa ziara yake ya siku mbili nchini Algeria ambayo imemalizika leo Alhamis.





Ziara hiyo imeweka alama ya kupigwa hatua katika kuweka nguvu zaidi ya ushirikiano wa kirafiki baina ya mataifa hayo mawili, kansela amesema baada ya mazungumzo na rais Abdelaziz Bouteflika.

Waliohudhuria mazungumzo hayo ni pamoja na waziri wa nishati na migodi wa Algeria Chakib Khelil ambaye ni rais wa sasa wa mataifa yanayosafirisha kwa wingi mafuta , OPEC, naibu waziri wa ulinzi Abdelmalek Guenaizia, waziri wa mambo ya kigeni Mourad Medelci pamoja na waziri wa mawasiliano ya simu Hamid Bessallah.

Licha ya kuwa ni mkataba mmoja tu muhimu ndio uliotiwa saini , wa kujenga msikiti mkubwa kabisa ambao utakuwa na uwezo wa kuingiza waumini 40,000 kwa wakati mmoja , viongozi wa makampuni ambao walifuatana na kansela Merkel wameeleza matumaini yao ya kutiwa saini makubaliano mengine zaidi.

Wakati wa ziara hiyo, jopo la kundi la viongozi wa makampuni na wawakilishi wa serikali kutoka kila upande liliundwa ili kuimarisha mahusiano ya kiuchumi.

Makampuni ya Ujerumani yanakodolea macho hifadhi kubwa ya fedha za kigeni za Algeria pamoja na hifadhi kubwa ya mafuta na gesi ya ardhini nchini humo.

Mkataba wa ujenzi wa msikiti , ambao ni wa kujenga msikiti wa tatu kwa ukubwa duniani mjini Algiers ulitiwa saini wakati wa ziara hiyo.

Wasanifu majengo wa Ujerumani Engel na Zimmermann, pamoja na wahandishi wa ujenzi Krebs na Kiefer, watajenga msikiti huo kwa gharama ya Euro bilioni moja katika muda wa miaka minne ijayo baada ya kupata kandarasi hiyo mwaka jana.

Miongoni mwa kandarasi ambazo bado zinafikiriwa ni za kutengeneza manowari nne kwa ajili ya jeshi la majini la Algeria kwa gharama ya kiasi cha Euro bilioni 5.

Biashara baina ya Ujerumani na Algeria ilikuwa inafikia kiasi cha Euro bilioni 1.2 mwaka 2007. Merkel amesema kuwa inawezekana kuongeza kiasi hicho.

Ekkehard Schutz mwenyekiti wa bodi ya kampuni linalotengeneza vifaa vya chuma ThyssenKrupp, ametabiri kupanda kwa biashara baina ya mataifa hayo, ambapo taifa hilo la Afrika ya kaskazini kuwa eneo muhimu kwa Ujerumani.

Makampuni ya nishati ya Ujerumani E.on na RWE yanataka mikataba ya mafuta na gesi, na iko mipango ya kuunda kinu cha kufua umeme kitakachotumia nishati ya gesi ya ardhini na jua. Ujerumani ni miongoni mwa viongozi katika teknolojia ya nishati ya jua.

Wakati huo huo kansela Angela Merkel alitumia wakati wa maadhimisho yake ya miaka 54 ya kuzaliwa leo kuelezea kuunga kwake mkono wanawake wa Algeria katika mapambano yao ya usawa.