1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky: Urusi kuzidisha mashambulizi, Ukraine

3 Januari 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Urusi inajiandaa kuzidisha mashambulizi yake nchini Ukraine ikitumia ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa na Iran.

https://p.dw.com/p/4LhAr
Ukrainie | Präsident Selenskyj
Picha: Ukrainian Presidency/abaca/picture alliance

Baada ya vikosi vya Ukraine kusababisha vifo vya wanajeshi 63 wa Urusi katika mkesha wa mwaka mpya katika mji wa Makiivka mashariki mwa Ukraine, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema katika hotuba yake ya usiku wa kuamkia leo kuwa wanazo taarifa ya kwamba Urusi inapanga mashambulizi ya muda mrefu kwa kutumia ndege zisizo na rubani na zinazolipuka maarufu kama Shaheds.

Ukraine Kiew | Wolodymyr Selenskyj, Präsident
Volodymyr Zelensky, Rais wa UkrainePicha: Ukrainian Presidential Press Office/AP Photo/picture alliance

"Tuna habari kwamba Urusi inapanga mashambulizi ya muda mrefu kwa kutumia ndege zisizo na rubani za "Shaheds". Inalenga kutuchosha,  inalenga uchovu wa watu wetu, inalenga mifumo yetu ya ulinzi wa anga na sekta yetu ya nishati. Lakini tunahakikisha kuwa tutafanya kila liwezekanalo ili lengo hili la magaidi lishindwe kama yalivyoshindwa mengine yote."

Soma zaidi: Urusi yakiri kupoteza zaidi ya wanajeshi 60

Aidha, Zelensky ameonya kwamba katika wiki zijazo, usiku unaweza kutokuwa na utulivu kabisa na kuongeza kuwa katika siku mbili za kwanza za mwaka mpya, zilizogubikwa na mashambulizi ya usiku ya ndege zisizo na rubani kwenye miji ya Ukraine na miundombinu ya nishati, vikosi vya Ukraine vilidungua ndege zipatazo 80 zisizo na rubani zilizotengenezwa na Iran.

 

Vita vyenye dosari

Russland Putin Ansprache Neujahr
Rais wa Urusi Vladimir Putin akiwa na wanajeshi wakePicha: Kremlin/AA/picture alliance

Rais wa Urusi Vladimir Putin analenga kurejesha kasi katika vita vyake vyenye dosari, ambapo katika miezi ya hivi karibuni, juhudi zake zimekuwa zikidhoofishwa na mashambulizi ya Ukraine ambayo kwa kiasi fulani yamefanikiwa kutokana na msaada mkubwa wa silaha zinazoendelea kutolewa na Mataifa ya Magharibi. Hilo limezusha hasira miongozi mwa Warusi wenyewe pamoja na kauli za kukemea utendaji wa jeshi la Moscow.

Soma zaidi:Urusi yajiandaa kwa mashambulizi zaidi Ukraine 

Katika kudhihirisha hasira yao juu ya tukio hilo, baadhi ya wabunge na hata makundi ya Urusi yenye misimamo mikali ya utaifa, wametaka makamanda wapewe adhabu wakiwatuhumu kupuuza hatari iliyokuwepo.

Bilderchronik des Krieges in der Ukraine | Makijiwka
Magari yakiteketea kwa moto baada ya makombora kushambulia kituo cha ghala la mafuta katika eneo linalodhibitiwa na wanajeshi wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi huko Makiivka, Donetsk, mashariki mwa Ukraine, Mei 4, 2022.Picha: AP Photo/picture alliance

Katika tukio la hivi karibuni ambalo ni aibu kwa Kremlin, ni la vikosi vya Ukraine kurusha makombora katika kituo kimoja mashariki mwa mkoa wa Donetsk na kuwaua wanajeshi wa Urusi wapatao 63. Katika tukio la nadra, wizara ya ulinzi ya Urusi ilithibitisha taarifa hiyo ambayo ilikuwa ni moja ya mashambulizi mabaya zaidi kwa vikosi vya Urusi tangu ilipoivamia Ukraine zaidi ya miezi 10 iliyopita.

 

Msaada zaidi kwa Ukraine

Deutschland I G7-Gipfel in Elmau
Waandamanaji wakipinga uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, Juni 26,2022Picha: Alexandra Beier/AP/picture alliance

Daima kuhusiana na mzozo huo, baadhi ya waandamanaji nchini Ujerumani, iwe mitandaoni au mitaani, wametoa wito kwa Berlin kufikiria upya msaada wake kwa Ukraine, huku wakiunyooshea kidole uhusiano uliyokuwepo kati ya Umoja wa KiSoviet na Ujerumani ya Mashariki ya Kikomunisti na miongo kadhaa ya utegemezi wa Ujerumani kwa gesi ya Urusi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakati akimpokea Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson mjini Paris, amethibitisha kwa mara nyingine leo kwamba Ukraine inahitaji msaada zaidi kuliko hapo awali.