1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky, Macron, Merkel wazungumzia Ukraine mashariki

16 Aprili 2021

Rais Volodymyr Zelensky amefanya mazungumzo na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, huku kukiwa na taharuki kwa hatua ya Urusi kutuma wanajeshi wake kwenye mpaka wake na Ukraine.

https://p.dw.com/p/3s8V1
Ukraine Präsident Wolodymyr Selenskyj | Mimik
Picha: Janek Skarzynski/AFP/Getty Images

Zelensky na mkewe Olona waliwasili mchana wa Ijumaa (16 Aprili) kwenye Kasri la Elysee na kulakiwa Macron na mkewe, Brigitte, kabla ya viongozi hao wawili kufanya mkutano kwa njia ya vidio na Kansela Merkel akiwa Berlin. 

Kwenye mahojiano yake na gazeti la Le Figaro la Ufaransa, Zelensky alisema umefika wakati wa kuacha kuzungumza na umewadia wa kufanya maamuzi," akisisitiza kwamba mazungumzo ya leo yanajikita makhsusi kwenye mambo ya kiusalama.

Jana Zelensky aliongoza kikao cha baraza la usalama la nchi yake, akisema kwamba majadiliano mjini Paris yangelikuwa muhimu kwenye kuandaa kile alichokiita mazungumzo ya "Mfumo wa Normandy" yanayowahusisha viongozi wakuu wa Ukraine, Ufaransa, Urusi na Ujerumani.

Mazungumzo hayo yalifanyika wakati Ukraine na washirika wake wa Magharibi wakionesha wasiwasi wao kufuatia Urusi kuimarisha vikosi vyake kwenye mpaka wake upande wa mashariki mwa Ukraine.

Marekani na Jumuiya ya Kujihami ya NATO zinasema kuwa uimarishaji wa mara hii ni mkubwa kabisa tangu ule wa mwaka 2014.

Urusi kujibu vikwazo vya Marekani

USA Russland Kombo Joe Biden und Putin
Picha: Eric Baradat/Pavel Golovkin/AFP

Kwa upande mwengine, Urusi ilisema kuwa baina yake na Marekani hapana maeleweano yenye manufaa kwa pande zote mbili na kwamba Rais Putin atachukuwa hatua za kukabiliana na vikwazo vya Marekani.

Kauli hiyo ilitolewa siku ya Ijumaa (Aprili 16) na msemaji wa ikulu ya Krelmin, Dmirty Peskov, siku moja baada ya Marekani kutangaza vikwazo vipya dhidi ya Urusi, vikiwemo vile vinavyohusu kuzuwia deni lake la nje.

Marekani imechukuwa hatua hiyo hata baada ya hivi juzi Rais Joe Biden kuomba mkutano wa ana kwa ana na Rais Putin, kulainisha uhasama wao na hasa kuhusu kinachoendelea mashariki mwa Ukraine.

"Biden ametowa mapendekezo mengi. Lakini mapendekezo hayo yanagongana na hatua za sasa. Bila shaka, itachukuwa muda kuchambua pendekezo la sasa, na kwa mujibu wa maamuzi ya mkuu wa nchi, jibu litatolewa baada ya Rais wa Urusi kufanya maamuzi yake." Alisema Peskov mbele ya waandishi wa habari mjini Moscow.

Zaidi ya watu 14,000 wameshakufa katika mapigano ya miaka saba sasa kati ya wanajeshi wa Ukraine na waasi wanaoungwa mkono na Urusi mashariki mwa Ukraine, ambayo yalianza mara tu baada ya Urusi kuitwaa Rasi ya Crimea, ambayo hadi leo inatambuliwa kimataifa kuwa sehemu ya Ukraine.

Juhudi za kusaka suluhisho la kisiasa zimekwama na uvunjwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano umekuwa ukiongezeka katika wiki za hivi karibuni katika eneo lote la ukanda wa mashariki mwa Ukraine, lifahamikalo kama Donbas.