1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky: Pasaka ijayo itakuwa huru na amani kwa Waukraine

Hawa Bihoga
10 Aprili 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameshutumu mashambulizi ya anga ya Urusi yalioangukia maandalizi ya Pasaka ya wa Orthodox siku ya Jumapili, ikiwa ni pamoja na lile lililowauwa baba na binti yake huko Zaporizhzhia.

https://p.dw.com/p/4PraE
Ukraine Kiew | Präsident Wolodymyr Selenskyj
Picha: Genya Savilov/AFP

Katika utaratibu wake wa kulihutubia taifa kila jioni na siku muhimu kwa Waukraine, Zelensky amesema usiku wa kuamkia leo, jeshi la Urusi lilishambulia huko Zaporizhzhia kwa makombora ya S-300.

Katika mfululizo wamakombora yaliopiga katika makaazi ya raialikiwemo jengo la ghorofa nne, watu watatu waliuawa - mwanaume mwenye umri wa miaka 50, mwanamke na mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 11.

"Hivi ndivyo serikali ya kigaidi inavyoadhimisha sikukuu hii leo Jumapili." Alisema Zelensky katika video ya hotuba yake ikiwa ni maadhimisho ya sherehe muhimu ya waumini wa madhehebu ya Orthodox ambao siku ya Jumapili wanaadhimisha makaribisho ya Yesu yaliofanywa na wakaazi wa Jerusalem, ikiwa ni wiki moja kabla ya kusherehekea Pasaka yao.

Soma pia:Papa arejea wito wa kustishwa mapigano Ukraine

Rais Zelensky amevipongeza vikosi kadhaa vinavyolinda maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo, akisema ana matumaini makubwa katika sherehe kama hizo mwaka ujao Ukraine itakuwa huru.

"Natumaini mwaka ujao sherehe itafanyika kwa uhuru na amani kwa watu wetu wote."

Waukraine takribani milioni 41 ni waumini wa madhehebu ya Orthodox ambao husherehekea sikukuu ya Pasaka wiki moja kutoka sasa.

Mashambulizi ya Moscow yajibiwa

Mkuu wa majeshi wa Ukraine amesema katika ripoti yake kwamba, zaidi ya mashambulizi 40 ya adui yamezuiliwa katika muda wa masaa 24 yaliyopita.

Ukraine Krieg | Ukrainische Soldaten bei Bachmut
Askari jeshi wa Ukraine wakiwa katika uwanja wa vita BakhmutPicha: Diego Herrera Carcedo/AA/picture alliance

Mkuu huyo ameongeza kuwa majeshi ya Urusi yalianzisha mashambulizi ambayo hayakufanikiwa katika maeneo ya magharibi mwa Bakhmut ambayo imeharibiwa kwa kiwango kikubwa.

Taarifa hiyo imesema kuwa Urusi pia haijafanikiwa mashambulizi yake huko Avdiivka, eneo jengine la kimkakati ambalo linalengwa na vikosi vya Urusi katika uwanja wa mapambano mashariki mwa Ukraine.

Vikosi vya Ukraine vimesema vitaendelea kuilinda Bakhmut dhidi ya mashambulizi ya mara kwa mara ya Urusi, ingawa wiki iliyopita Rais Zelensky alikiri kwamba kuna hatari ya vikosi vyake kuzingirwa na kurudishwa nyuma.

Soma pia:Ukraine yaendelea kuipigania Bakhmut

Msemaji wa jeshi upande wa Mashariki mwa Ukraine, Serhiy Cherevatyi, aliiambia televisheni ya taifa kwamba "vikosi vya Urusi vinajaribu kuchukua himaya ya jiji letu kwa gharama yoyote", akiongeza kuwa mapambano bado ni makali na wanaendelea na udhibiti wa mji huo wa kimkakati.

"Vikosi vyetu vinamrudisha nyuma adui na kumetokea uharibifu mkubwa."

Urusi yasema imeharibu maghala ya mafuta, silaha

Katika hatua nyingine wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema vikosi vyake vimeharibu ghalalililokuwa na tani 70,000 za mafuta karibu na Zaporizhzhia pamoja na maghala mengine ya kuhifadhi makombora, risasi na silaha huko Zaporizhzhia na Mikoa ya Donetsk.

Hata hivyo, taarifa hizo hazikuthibitishwa mara moja na Kyiv na badala yake wamesisitiza katika kuendelea kupigania mipaka yake kwa uhuru wa Ukraine na watu wake hadi kufikia maadhimisho ya siku kuu ya Pasaka ijayo.