1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 800,000 wameabukizwa corona barani Afrika

Zainab Aziz Mhariri: Tatu Karema
25 Julai 2020

Idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona barani Afrika imepindukia watu 800,000. Wakati huohuo WHO imeelezea wasiwasi wake kuhusu kuzuka upya kwa mripuko wa virusi vya corona barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/3fu4Y
Schweiz, Genf I Hauptsitz der Weltgesundheitsorganisation I WHO I Gebäude
Picha: Reuters/D. Balibouse

Kwa mujibu wa taarifa ya wakala wa afya wa Jumuiya ya Afrika inayosimamia vituo vya kudhibiti na kuzuia magonjwa barani humo, CDC, Afrika Kusini ndio inaongoza kwa kuwa na nusu ya idadi iliyotajwa ya watu walioambukizwa katika jumla ya mataifa 54 yaliyopo barani Afrika.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba viwango vya maambukizi vinaongezeka kwa kasi katika mataifa mengine barani humo na imeitaja Kenya iliyo na zaidi ya watu elfu 16 waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya corona mpaka sasa. Bara la Afrika limekuwa likiwekewa hofu kabla ya hata kuripotiwa maambukizi ya kwanza barani humo yaliyothibitishwa mnamo Februari 14.

Katika tamko lake kuhusu hali ya dharura ya afya duniani kote mnamo mwezi Januari, Shirika la afya duniani WHO lilisema bara la Afrika lingeathirika zaidi na janga la corona kutokana na kuwepo mifumo duni ya huduma za afya.Wataalamu wa afya wametahadharisha kwamba huenda janga la COVID -19 likaendelea kuwepo kwenye baadhi ya nchi za Afrika kwa muda mrefu.

Mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Getty Images/Afp/F. Coffrini

Wakati huo huo shirika la afya duniani WHO limeelezea wasiwasi wake kuhusu kuzuka upya kwa mripuko wa virusi vya corona barani Ulaya baada ya Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Austria kutangaza sheria kali za kuvaa barakoa na kusisitiza juhudi za kuwapima watu kwa wingi.

Bara Ulaya linajumuisha humusi moja ya maambukizi ya zaidi ya milioni 15 ya virusi vya corona kote duniani na linaendelea kuwa eneo lililoathirika zaidi kutokana na watu waliokufa kutokana na COVID -19.  Bara Ulaya lina watu 207 118 waliothibitishwa kuwa wameambukizwa virusi vya corona kati ya jumla ya watu 630 000 walioambukizwa kote duniani tangu kuzuka mara ya kwanza kwa virusi hivyo nchini China mwishoni mwa mwaka jana.

Shirika la afya duniani WHO limetaja kuongezeka kwa maambukizi kote barani Ulaya katika muda wa kipindi cha wiki mbili zilizopita na limesema hatua kali zaidi huenda zitahitajika kukabiliana na kuenea kwa virusi nya corona.

Vyanzo:/AP/AFP