1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBangladesh

Yunus: Bangladesh imejipatia uhuru kwa mara ya pili

8 Agosti 2024

Muhammad Yunus aliyewasili Bangladesh leo akitokea Ufaransa alikokuwa anapokea matibabu anatarajiwa kuchukua rasmi madaraka wakati akitarajiwa pia kurejesha utulivu na kuijenga upya nchi hiyo kufuatia maandamano makubwa.

https://p.dw.com/p/4jGLV
Muhammad Yunus
Mshindi wa Tuzo ya Nobel Muhammad Yunus (katikati) akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hazrat Shahjalal mjini Dhaka mnamo Agosti 8, 2024.Picha: Munir Uz Zaman/AFP

Kauli yake ya kwanza aliyoitoa baada ya kuwasili Bangladesh akitokea mjini Paris Ufaransa, Yunus, amewaambia waandishi wa habari kwamba, kipaumbele chake ni kurejesha hali ya utulivu.

Akiandamana na baadhi ya viongozi wa wanafunzi walioongoza maandamano dhidi ya serikali iliopita, Yunus amesema Bangladesh ni familia moja na lazima wananchi waungane na kuwa kitu kimoja.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 84 ameeleza kuwa leo ni siku muhimu katika historia ya Bangladesh.

Soma pia: Nguvu ya vijana yaanguasha utawala wa miaka 15 Bangladesh

Amesema nchi hiyo imeunda kile alichokiita "siku mpya ya ushindi." Kiongozi huyo amekwenda mbali zaidi na kusema Bangladesh imejipatia uhuru kwa mara ya pili.

Aidha ametoa mwito wa kurejeshwa kwa hali ya utulivu kufuatia wiki kadhaa za maandamano ya vurugu yaliyosababisha vifo vya watu 455. Yunus ambaye ataongoza serikali ya mpito amewahimiza wananchi kuchukua jukumu la kuwalinda wenzao, wakiwemo jamii ya walio wachache waliokuwa wakilengwa wakati wa maandamano.

"Mumeweka imani yenu kwangu, nyinyi pamoja na wanafunzi mumeniita, na nikaitikia wito wenu. Ombi langu kwenu ni kama mumeweka imani yenu kwangu, kama munanitegemea, basi hakikisheni hakuna mashambulizi yanayolenga mtu yoyote, popote alipo nchini."

Kuna uwezekano mkubwa kwa Yunus kuapishwa kuwa kiongozi mpya wakati wowote kutoka sasa.

Mtangulizi wake, Sheikh Hasina anayeshutumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kuwafunga jela wapinzani wake wa kisiasa, alilazimika kukimbilia nchi jirani ya India siku ya Jumatatu.

Yunus awapongeza vijana kwa kulipa taifa uhai mpya

Muhammad Yunus akiapishwa kama mshauri mkuu wa serikali mpya ya mpito ya Bangladesh mjini Dhaka mnamo Agosti 8, 2024, wakati Rais Mohammed Shahabuddin akisimamia hafla ya kula kiapo
Muhammad Yunus akiapishwa kama mshauri mkuu wa serikali mpya ya mpito ya Bangladesh mjini Dhaka mnamo Agosti 8, 2024, wakati Rais Mohammed Shahabuddin akisimamia hafla ya kula kiapoPicha: MUNIR UZ ZAMAN/AFP

Baada ya Hasina kuikimbia nchi, jeshi liliitikia wito wa wanafunzi wa kumtaka Yunus ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2016, kuongoza serikali ya mpito.

Alipowasili mjini Dhaka, Yunus aliamsha hisia za Wabangladesh kwa kusimulia mauaji ya kikatili ya mwanaharakati mwanafunzi Abu Sayeed, aliyepigwa risasi na polisi mwezi uliopita.

Kiongozi huyo amewapongeza vijana kwa kuongoza maandamano yaliyobadili mkondo wa taifa, kwa kusema maandamano hayo yalilipa taifa uhai mpya.

Soma pia: Serikali ya mpito Bangladesh kushirikisha makundi yote 

Wakati wa utawala wa Hasina, Yunus alikabiliwa na zaidi ya kesi 100 za uhalifu na kupakwa tope na serikali iliyopita iliyomtuhumu kwa kupigia debe ushoga na mapenzi ya jinsia moja.

Wakati hayo yakijiri, gazeti la Prothom Alo limeripoti kuwa viongozi wa wanafunzi walioongoza maandamano Nahid Islam na Asif Mahmud, pia watakuwa sehemu ya serikali mpya ya mpito.