1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yanayoendelea nchini Syria

30 Aprili 2018

Jeshi la Syria leo limelishambulia kwa mabomu eneo mojawapo la waasi huku makubaliano ya kuwaondoa waasi hao yakiwa yamefikiwa na rais Assad anaendeleza mkakati wa kuikomboa ngome ya mwisho ya waasi.

https://p.dw.com/p/2ww42
Syrien Schiitische Gruppen
Picha: picture-alliance/AP Photo/J.al-Helo

Vyombo vya habari vya serikali vya nchini Syria vimearifu juu yakufikiwa makubaliano juu ya kuwahamisha wapiganaji wanaohusishwa na kundi la al-Qaida kutoka kwenye kambi ya wakimbizi wa Kipalestina iliyopo karibu na mji wa Damascus, na kisha badala yake kuachiwa huru watu kadhaa waliokuwa wanashikiliwa na waasi kwa miaka mingi.

Mgogoro wa Syria
Mgogoro wa SyriaPicha: picture alliance/XinHua/dpa/A. Safarjalani

Mapema leo jeshi la Syria liliushambulia kutoka angani mji wa Rastan na vijiji vilivyo karibu na miji ya waasi ya Hama na Homs. Kwa mujibu wa Shirika linalo tetea Haki za Binadamu nchini Syria majeshi ya serikali yamefanya mashambulizi ya anga zaidi ya 140.

Waasi wa Syria wanashikilia maeneo makubwa huko kaskazini magharibi na kusini magharibi mwa Syria. Muungano wa wanamgambo wa Kikurdi na ule wa Kiarabu unaoungwa mkono na Marekani unadhibiti sehemu kubwa za kaskazini na mashariki mwa Syria.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike PompeoPicha: Imago/C. May

Akizungumza huko Israeli hapo jana Jumapili, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alisema nchi yake ina wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka kwa vitisho vya Iran dhidi ya Israel na kanda ya mashariki ya kati na kwamba ni muhimu kwa  Marekani na Israel, washirika hao wawili kufanya kazi kwa pamoja ili kuizuia Iran.

Wanadiplomasia wameonya kuhusu uhasama unaoendelea kukua kati ya Israeli na Iran huko nchini Syria wakati ambapo rais Assad na washirika wake wakiendelea kuyakomboa maeneo zaidi yanayodhibitiwa na waasi.

Takriban watu 26 waliuwawa baada kambi ya kijeshi kaskazini mwa Syria kushambuliwa kwa roketi ambapo awali ilitangazwa kuwa kati ya watu hao waliouwawa walikuwemo wapiganaji raia wa Iran lakini Iran imekanusha madai hayo.

Majeshi ya Syria na pembeni picha ya rais Bashar al Assad
Majeshi ya Syria na pembeni picha ya rais Bashar al AssadPicha: Getty Images/AFP/G. Ourfalian

Mpaka sasa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na mashambulizi ya makombora dhidi ya kambi kadhaa za majeshi ya serikali ya Syria licha ya kuwepo tetesi kwamba Israel imehusika na mashambulizi hayo ambayo yanatishia kuupalilia  zaidi  mgogoro huo wa miaka saba.

Mwandishi:Zainab Aziz/RTRE/APE

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman