1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Wizara ya muungano ya Korea Kusini yapata ugumu Kaskazini

28 Julai 2023

Mteule wa kihafidhina wa Korea Kusini anaetazamiwa kuwa Waziri wa Muungano amesema anataka kuishinikiza Pyongyang juu ya ukiukwaji wa haki na kuachana na sera ya kutaka kujiridhisha iliyofuatwa na serikali iliyopita.

https://p.dw.com/p/4UWHo
Südkorea Seoul | Anhörung zur Bestätigung von Kim Yung-ho als Minister für Wiedervereinigung
Waziri mpya wa Muungano wa Korea Kusini, Kim Yung-hoPicha: Yonhap/picture alliance

Korea Kaskazini na Kusini zimeadhimisha miaka 70 tangu kusitishwa kwa vita baina yao vilivyodumu kwa miaka mitatu, ingawa uhasama wa wazi kati ya pande hizo mbili bado upo hadi leo. 

Mabadiliko ya hivi majuzi yaliyofanywa na Rais Yoon Suk-yeol wa Korea Kusini kwa kumuingiza Kim Yung-ho serikalini yanasisitiza kuwa pengo linaongezeka kati ya pande hizo mbili.

Kim Yung-ho ni msomi wa kihafidhina ambaye aliwahi kusema kwamba taifa linahitaji kuwa na msimamo thabiti zaidi na Pyongyang, hasa inapokuja rekodi ya Kaskazini juu ya ukiukaji wa haki za binaadamu, kwa kuwepo wizara inayoratibu sera ya Korea Kusini kuelekea Kaskazini na kuweka sheria za ushirikiano.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya vikao vyake vya uthibitisho, Yung-ho alisema Seoul inapaswa kufanya chaguo na kuamua endapo  inapaswa kuendelea kuzingatia makubaliano yaliyofanywa na Korea Kaskazini chini ya serikali za awali za mrengo wa kushoto. 

Soma zaidiKorea Kaskazini yarusha makombora mawili, baada ya nyambizi ya Marekani kuwasili Korea Kusini 

Kwa kiongozi huyo mpya, ambaye amekosowa vikali urushaji wa makombora uliofanyika Kaskazini, majibu ya Seoul yanapaswa kuendana tabia ya jirani yake huyo. 

''Korea Kaskazini imeisaliti nia yetu njema kwa ajili ya amani ya Peninsula ya Korea na mustakabali wa watu wetu na imerudisha makubaliano mengi kati yake na Korea Kusini. Tunahitaji kuzidumisha kanuni zetu dhidi ya chokochoko za Korea Kaskazini na kujibu kwa ukali," alisema.

Yung-ho, anayetarajiwa kushika nafasi ya uwaziri wa sera ya muungano, ameeleza mipango yake ya kuipeleka wizara hiyo katika mwelekeo mwingine. 

Upi mtazamao wa Rais Yoon?

Ukraine Südkoreanischer Präsident Yoon Suk Yeol trifft Selenskyj in Kiew
Rais wa Korea Kusini Yoon Suk YeolPicha: Jae C. Hong/AP Photo/picture alliance

Mtazamo wake unalingana vyema na ule wa Rais Yoon, ambaye amechukua mkondo mkali zaidi dhidi ya utawala wa Kim Jong Un wa Korea Kaskazini kuliko mtangulizi wake, Moon Jae-in. 

Yoon, ambaye amesema kuwa wizara hiyo imekuwa ikifanya kazi "kama wakala wa usaidizi wa Korea Kaskazini," anataka kuelekeza upya malengo yake kwenye uhuru na demokrasia kwa raia wa Kaskazini.

Wizara ya muungano iliyoboreshwa zaidi inatarajiwa kuelekeza nguvu zake katika kufuatilia na kuorodhesha ukiukaji wa haki za binaadamu huko Kaskazini, na kuchanganua mienendo ya kisiasa na kubuni majibu mwafaka kutoka katika serikali ya Korea Kusini.

Mabadiliko ya kimuundo ya wizara pia yatapelekea kupunguzwa kwa idadi ya wafanyakazi wake wa sasa  616, japo inaonekana huenda itapoteza hadhi yake kama wizara huru na kujumuishwa kama wakala wa wizara ya mambo ya nje. 

Idara moja ambayo huenda ikaondolewa ni Kaesong Industrial District Foundation, ambayo ilishtakiwa kwa kusimamia kampuni za Korea Kusini ambazo zilikuwa na shughuli ndani ya Kaesong Industrial Complex, kituo cha pamoja cha utengenezaji bidhaa baina ya Kaskazini na Kusini kilichoanzishwa karibu na mpaka wa Korea Kaskazini mwaka 2002 ikiwa ni hatua ya kujengeana imani.

Soma zaidi:Marekani na Korea Kusini zatafakari kutanua Luteka za Kijeshi 

Serikali ya Korea Kusini ilijiondoa katika mradi huo baada ya Korea Kaskazini kurusha roketi mwaka wa 2016, na kuripua ofisi ya mawasiliano kwenye eneo hilo.

Park Jung-won, profesa wa sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Dankook, anaamini kuwa serikali iliyopita iliitumia vibaya wizara hiyo kwa vile ilitoa usaidizi kwa serikali ya Korea Kaskazini tu na haikupokea malipo yoyote, kama vile hatua za kuondoa silaha za nyuklia.

Akizungumza na DW, amesema mabadilishano yote yanapaswa kufaidisha maslahi halisi ya Korea zote mbili, badala ya kuunga mkono tu serikali ya Korea Kaskazini. 

"Wizara inapaswa kupata faida kama vile kuboreshwa kwa rekodi ya haki za binaadamu na mikutano kati ya familia ambazo zimegawanyika tangu kumalizika kwa vita vya Korea mwaka 1953," alisema msomi huyo.

Park anadokeza kuwa wizara hiyo kwa ufanisi imekuwa na machache ya kufanya tangu mkutano wa Hanoi wa Februari 2019, ambao ulivunjika wakati rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, alipotoka baada ya Kim kutaka vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wake viondolewe.

Korea Kaskazini yakataa kufanya mawasiliano na Korea Kusini

Tangu wakati huo, Kaskazini imekataa kuwasiliana na Kusini, hata kwa kujibu maombi kutoka kwa serikali inayoendelea ya rais wa zamani, Moon.

Naye Kim Sang-woo, mwanasiasa wa zamani wa chama cha mrengo wa kushoto cha Korea Kusini, ambaye kwa sasa ni mjumbe wa bodi ya Wakfu wa Amani wa Kim Dae-jung, anasema Rais Yoon "amechanganyikiwa" kwa kuwa serikali iliyopita imekuwa ikishughulikia masuala ya Kaskazini, lakini hakuna matokeo chanya.

"Wizara ya muungano imekuwa kama duka lililokufa, basi Yoon ataipunguza jukumu lake, ikiwezekana ataiweka chini ya wizara ya mambo ya nje kama wakala," aliongeza.

Nordkorea | Südkorea | DMZ an der Grenze in Panmunjom
Daraja Kuu la Muungano lililopo PanmunjomPicha: Kim Hong-Ji/REUTERS

Mwanasiasa huyo anaamini Yoon yuko kihafidhina zaidi na ameweka wazi kuwa yuko tayari kwa mazungumzo iwapo Kaskazini itakuja na nia njema, lakini ikiwa sivyo, basi hataomba mazungumzo.

Uhusiano kati ya pande hizo mbili umeendelea kuzorota katika miaka ya hivi karibuni na Sang-wo hajui ikiwa msimamo mkali kuhusu rekodi ya haki za binadaamu ya Kaskazini utakuwa wa manufaa.