1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Korea Kusini huenda zitatanua Luteka za Kijeshi

21 Mei 2022

Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol wamesema huenda watatafakari kutanua luteka ya kijeshi ya kila mwaka kama njia ya kudhibiti kitisho kutoka Korea Kaskazini.

https://p.dw.com/p/4Bg8f
Südkorea Seoul | Yoon Suk-yeol, Präsident & Joe Biden, US-Präsident
Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Biden na Yoon walikuwa wakizungumza na waandishi habari baada ya kufanya mazungumzo mjini Seoul katika siku ya pili ya ziara ya Biden nchini Korea Kusini.

Matamshi hayo wameyatoa katika wakati hakuna ishara ya kufanikiwa kwa njia za kidiplomasia kuizuia Korea Kaskazini kuendeleza mradi wake wa silaha za nyuklia ambao umekuwa kitovu cha mvutano wake na Jumuiya ya Kimataifa pamoja na jirani yake wa rasi ya Korea.

Tangazo la viongozi hao wawili linaakisi mabadiliko makubwa ya mwelekeo wa kisera tofauti na watangulizi wao.

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ilikuwa nusura afikie uamuzi wa kusitisha mazoezi hayo ya kijeshi ya  ila mwaka na Korea Kusini baada ya kustawi kwa mahusiano kati yake na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.

Kadhalika rais aliyeondoka madarakani hivi karibuni nchini Korea Kusini, Moon Jae-in alichukua msimamo wa kutaka kuendeleza mazungumzo na Kim licha ya kupuuzwa kila wakati na watawala wa mjini Pyongyang.

Biden asifu mahusiano ya Marekani na Korea Kusini

Biden amesema ushirikiano kati ya Marekani na Korea Kusini unaonesha "utayari wetu wa kushughulikia vitisho vyote kwa pamoja."  

Südkorea USA Militärmanöver
Luteka ya Kijeshi ya kila mwaka kati ya Marekani na Korea Kusini hukosolewa na Korea Kaskazini Picha: Jung Yeon-Je/AFP

Korea Kaskazini imekuwa ikitetea mpango wake wa nyuklia ikisema inauhitaji ili kujihakikishia usalama dhidi ya kile watawala wa nchi hiyo wanakitaja kuwa vitisho kutoka Marekani.

Tangazo la leo Jumamosi yumkini litazusha hasira mjini Pyongyang. Viongozi wa Korea Kaskazini wamekuwa wakisema mazoezi yao ya kijeshi ya kila mwaka ya Marekani na Korea Kusini ni matayarisho ya kuivamia nchi hiyo.

Washington na Seoul zinayapinga madai hayo zikisema luteka hiyo inaimarisha utayari wa kujilinda na siyo uchokozi.

Kwenye mkutano wa leo Biden na Yoon walisisisitza dhamira yao ya kuendelea kufanya kazi pamoja ili kufikia lengo la kuondoa silaha za nyuklia kwenye rasi ya Korea.

Wamesisitiza pia nia yao ya kuheshimu na kutumia "desturi za kimataifa zinazokubalika na wengi"  kushughulikia suala la Korea Kaskazini.

Biden kuitembelea Japan siku ya Jumapili 

Pamoja na suala la nyuklia, Biden amerejea dhamira yake ya kuipatia Korea Kaskazini chanjo ya virusi vya corona. Amesema Washington iko tayari hata kutuma shehena ya chanjo kupitia China iwapo hilo litawaridhisha viongozi mjini Pyongyang.

"Ndiyo, tuko tayari kutoa chanjo, siyo kwa Korea Kaskazini pekee lakini na kwa China pia. Tumejitayarisha kufanya hivyo haraka sana lakini bado hatujapokea majibu"amesema Biden.

Mbali ya suala la Korea Kaskazini viongozi hao wawili wamezungumzia mzozo nchini Ukraine, biashara kati ya nchi hizo mbili na kutanuka kwa ushawishi wa China.

USA Japan Biden Fumio Kishida Videokonferenz
Picha: Cabinet Secretariat/Kyodo News via AP/picture alliance

Hapo asubuhi Biden alianza siku ya pili ya ziara yake nchini Korea Kusini kwa kulitembelea eneo la makaburi ya askari Marekani na Korea Kusini waliopigana vita vya Korea. Hapo aliweka shada la maua na kusimama kwa dakika moja kuwakumbuka wanajeshi hao.

Hapo jana  alijiunga na mwenyeji wake, Rais Yoon Suk-yeol wa Korea Kusini, kukitembelea kiwanda cha bidhaa za elektroniki cha Samsung mjini Seoul ambako Biden alisema teknolojia ni moja ya jambo muhimu sana katika ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Siku ya Jumapili, Biden ataitembelea Japan ambako mbali ya mazungumzo na waziri mkuu Fumio Kishida atashiriki pia mkutano wa kundi la QUAD linalozijumuisha Marekani, Australia, India na Japan.