1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa amani watawala mkutano wa Umoja wa Afrika

18 Februari 2023

Viongozi wa mataifa ya Afrika wamekutana Jumamosi mjini Addis Abbaba katika siku ya kwanza ya mkutano wa kilele wa siku mbili utakaojadili kwa upana matatizo yanayolikumba bara hilo.

https://p.dw.com/p/4Ngw0
Äthiopien Hauptqartier der Afrikanischen Union in Addis Abeba
Makao Makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, EthiopiaPicha: Solomon Muchie/DW

Katika siku ya kwanza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewarai viongozi wa mataifa 55 wanachama wanaohudhuria mkutano huo kusaka amani kwenye maeneo yote yanayoandamwa na mizozo.

Bara hilo hivi sasa linashuhudia ukame usio mfano kwenye eneo la Pembe ya Afrika na wimbi la kutisha la machafuko kwenye kanda ya Sahel na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Mkutano huo wa siku mbili kwenye mji mkuu wa Ethiopia unalenga kuyaweka mezani masuala yote hayo na kujaribu kuyatafutia majawabu.

Ajenda nyingine muhimu ni kutafuta njia ya kuutekelea mkataba wa kanda huru ya kibiashara barani Afrika ambao tangu kuanza kwake kutekelezwa bado unasuasua.

Sehemu kubwa ya majadiliano ni ya faragha huku inaareifiwa kwamba zaidi ya marais 30 na mawaziri wakuu wa mataifa mbalimbali ya Afrika wanahudhuria.

Mzozo wa Kongo na machafuko huko Sahel ni ajenda za kipaumbele 

Macho ya wengi yatakuwa yakitazama iwapo Umoja wa Afrika unamudu kufanikisha usitishaji machafuko kwenye kanda ya Sahel ambayo imekumbwa na wimbi la hujuma za makundi ya itikadi kali za dini ya kiislamu. Mzozo wa mashariki ya Kongo pia utamulikwa kwa karibu.

Kwenye taifa hilo waasi wa M23 wamekamata maeneo makubwa ya ardhi na kuzusha mtafaruku wa kidiplomasia kati ya Kongo na jirani yake Rwanda, inayotuhumiwa kuwaunga mkono waasi hao.

Akuhutubia mkutano huo wa kilele Guterres ameirai Afrika kuchukua "mkondo wa amani", akisema bara hilo la waakazi bilioni 1.4 linakabiliwa na "vizingiti vikubwa kwenye kila nyanja".

UN-Generalsekretär  Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Picha: picture-alliance/ Pacific Press/L. Radin

"Nina wasiwasi mkubwa na kutanuka kwa hujuma za makundi ya watu wenye silaha mashariki mwa Kongo na makundi ya kigaidi huko Sahel na kwengineko" amesema Guterres kuuambia mkutano huo utakaoendelea hadi siku ya Jumapili.

"Mazingira ya kupata amani yanafifia" amesema mwanadiplomasia huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa alkini ameutolea mwito Umoja wa Afrika "kupambana kutafuta amani."

Kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa kilele viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inayojumuisha Kongo, walikutana pembezoni kwa majadiliano na kutoa azimio linaloyataka makundi yote yenye silaha kuondoka kwenye maeneo wanayoyashikilia mashariki mwa Kongo mwishoni mwa mwezi unaokuja.

Guterres naye kwa upande wake alikutana na viongozi kadhaa wa Afrika, ikiwemo rais Paul Kagme wa Rwanda, kwa majadiliano mahsusi kuhusu mzozo wa Kongo.

Rais wa Comoro achaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa AU 

Kombo-Bild Azali Assoumani (Präsident der Komoren), Macky Sall (Präsident Senegal)
Rais wa Comoro Azali Assoumani (kushoto) anakuwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika akimrithi Macky Sall wa Senegal (kulia) Picha: Kiyoshi Ota/Mast Irham/AP/picture-alliance

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huo ameumwagia sifa Umoja wa Afrika kwa kusaidia juhudi za upatanishi kati ya serikali yake na wapiganaji wa jimbo la kaskazini mwa nchi hiyi la Tigray.

Majadiliano hayo yaliwezesha kupatikana mkataba wa amani uliosaidia kumaliza vita vya miaka miwili kaskazini mwa Ethiopia.

Katika hatua nyingine mkutano huo umemchagua rais wa visiwa vya Comoro Azali Assoumani kuwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika katika kipindi cha mwaka mmoja.

Rais Assoumani anayeongoza nchi yenye idadi ya watu 900,000 alitumia hotuba yake ya kuridhia kuchaguliwa kutoa mwito wa "kufutwa kabisa" kwa deni la Afrika kutoka mataifa na taasisi za fedha za kimataifa.

Kiongozi huyo anayerithi mikoba kutoka kwa rais Macky Sall wa Senegal hakutoa ufafanuzi zaidi wa vipi hilo linaweza kufanikiwa.