1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WINDHOEK : Namibia yataka utulivu baada ya Nujoma

20 Machi 2005
https://p.dw.com/p/CFV9

Rais muasisi wa taifa la Namibia Sam Nujoma anan’gatuka hapo kesho na kitu ambacho wananchi wa Namibia wasingelikipendelea kabisa ni kukabidhiana madaraka kwa mizengwe.

Miaka 15 baada ya kuiongoza Namibia kufuatia kupata uhuru wake kutoka Afrika Kusini mpigania uhuru huyo wa enzi ya Vita Baridi anaikabidhi nchi ambayo licha ya matatizo yake imefurahia utulivu wa kisiasa na kiuchumi unaoonewa gere na nchi nyengine barani Afrika.

Nujoma ni mashuhuri mno miongoni mwa wananchi wake milioni moja na laki tisa ambao wamemchaguwa mrithi wake aliyemteuwa Hifikepunye Pohamba hapo mwezi wa Novemba na mamlaka yake ndani ya chama cha SWAPO yanaendelea kuwa na nguvu na hata kutiliwa mashaka.

Nujoma anatazamiwa kubakia kuwa mkuu wa SWAPO hadi mwaka 2007 jambao ambalo limezusha mashaka kwamba kunaweza kusababisha mkanganyiko na hata mapambano ya kuwania madaraka kama yale yalioshuhudiwa mwaka huu kati ya Rais wa zamani wa Malawi Bakili Muluzi na mrithi wake Bingu wa Mutharika.