1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani awasili Saudi Arabia

5 Septemba 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock ameitaka serikali ya Israel kutokataa tena kujadili suluhisho la mataifa mawili katika mzozo wa Palestina.

https://p.dw.com/p/4kIxj
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock na waziri mwenzake wa Saudia, Faisal bin Farhan Al Saud
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock na waziri mwenzake wa Saudia, Faisal bin Farhan Al SaudPicha: Thomas Koehler/AA/photothek.de/picture alliance

Akizungumza kwa uwazi kabla ya kuanza ziara yake ya 11 ya Mashariki ya Kati tangu vita vya Gaza vilipozuka, Baerbock amesema wajumbe wa serikali ya Israel ambao wanapinga kuhusu suluhisho la mataifa mawili kwa maneno na vitendo, wanahatarisha usalama wa muda mrefu wa Israel. Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Ujerumani ameonya kuwa mazungumzo ya aina hiyo ndiyo suluhisho pekee la amani ya kudumu, na njia pekee ya kupambana na ugaidi kwa muda mrefu.

Ziara ya Baerbock kuangazia juhudi za kusitisha mapigano

Baerbock ambaye amewasili Alhamisi kwenye mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh katika ziara yake ya Mashariki ya Kati atakwenda pia Jordan na Israel, kwa lengo la kufanya mazungumzo na viongozi wa kikanda kuhusu juhudi za kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza na kuachiliwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas.

Baerbock anatarajiwa Alhamisi kukutana na waziri mwenzake wa Saudia, Faisal bin Farhan Al Saud mjini Riyadh, kabla ya kuelekea Jordan kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje, Ayman al-Safadi, mjini Amman.

Hali ilivyo baada ya shambulizi la Israel karibu na mji wa Tubas
Hali ilivyo baada ya shambulizi la Israel karibu na mji wa TubasPicha: JAAFAR ASHTIYEH/AFP

Baada ya hapo atakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz, na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant Ijumaa, kabla ya ziara yake ya kuelekea Ramallah, katika Ukingo wa Magharibi, ambapo atafanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Palestina, Mohammed Mustafa.

Wakati huo huo shirika la Habari la Kipalestina, WAFA, limeripoti Alhamisi kuwa shambulizi la droni katika eneo la Tubas limewaua watu watano na kuwajeruhi wengine kadhaa.

Mashambulizi yaliyalenga maeneo ya magaidi

Jeshi la Israel limesema katika taarifa yake kwamba imefanya mashambulizi matatu yaliyoyalenga maeneo ya magaidi ambao wanahatarisha usalama wa wanajeshi, bila ya kutoa maelezo zaidi.

Mkaazi mmoja wa eneo hilo, Hanan Natour amesema jeshi la Israel limekuwa likiendeleza oparesheni zake bila kujali. ''Tangu kuanza kwa mashambulizi na jeshi la Israel kulivamia eneo hili, hofu imetanda, huku jeshi likiripua kila kitu bila kuzingatia kwamba kulikuwa na watoto,'' balifafanua Hanan.

Waandamanaji nchini Israel wakitaka kuachiwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas
Waandamanaji nchini Israel wakitaka kuachiwa kwa mateka wanaoshikiliwa na HamasPicha: Oren ZIV/AFP

Kwa zaidi ya muda wa wiki moja, mamia ya wanajeshi wa Israel wamekuwa wakifanya oparesheni mbaya zaidi katika Ukingo wa Magharibi, tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas.

Hamas: Netanyahu anakwamisha mpango wa amani

Ama kwa upande mwingine, Hamas imesema Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anajaribu kuzuia mpango wa kusitisha vita, baada ya Netanyahu kusema kundi hilo la Kipalestina limekataa kila kitu kilichowasilishwa katika mazungumzo. Kauli hiyo imetolewa wakati ambapo Netanyahu anakabiliwa na shinikizo la kimataifa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza, ambayo yatasaidia kuwachiliwa kwa mateka.

Huku hayo yakijiri, shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limesema kuwa oparesheni ya kiijeshi ya Israel huko Gaza inapaswa kuchunguzwa kama uhalifu wa kivita. Shirika hilo limesema siku ya Alhamisi kuwa jeshi la Israel limeharibu kinyume cha sheria ardhi ya kilimo na majengo ya raia, na kuharibu vitongoji vyote.

(AFP, DPA, AP, Reuters)