Waziri wa Fedha wa Marekani kujadiliana ´mazito´ na China
5 Aprili 2024Mazungumzo hayo yatajikita juu ya uzalishaji uliopindukia viwango wa viwanda vya China na mazingira magumu ya ushindani yanayozikabili kampuni za biashara za Marekani.
Yellen aliwasili siku ya Alhamisi kwenye mji wenye shughuli nyingi za biashara wa Guangzhou na hii leo amepangiwa kukutana na gavana wa jimbo la Guangdong uliko mji huo pamoja na Naibu Waziri Mkuu wa China, He Lifeng.
Huo ni mwendelezo wa jitihada za pande hizo mbili za kupunguza mivutano kwenye maeneo yote muhimu husasani biashara na masuala ya kijeshi.
Utawala wa rais Joe Biden unatiwa wasiwasi na uzalishaji wa kupita kiasi unaofanywa na makampuni ya China hasa kwenye uundaji wa vyombo na vifaa vya kielektroniki vinavyoliemea soko la dunia.
Yellen analenga kuwaambia maafisa wa China kuwa uzalishaji wa aina hiyo unayaumiza makampuni ya Marekani na nchi nyingine duniani na pia siyo rafiki kwa hatma ya viwanda vya nchi China.