1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tunisia: Vyama vya upinzani vyasusia uchaguzi wa Jumamosi

17 Desemba 2022

Watunisia leo Jumamosi wanapiga kura kuchagua bunge jipya. Hata hivyo vyama vya upinzani vinasema uchaguzi huo unaofanyika chini ya mageuzi ya kujilimbikizia mamlaka mikononi mwa Rais Kais Saied ni kinyume cha sheria.

https://p.dw.com/p/4L5Wy
Tunesien Tunis | Referendum zur Verfassung
Picha: ZOUBEIR SOUISSI/REUTERS

Vyama vya upinzani vimeamua kulisusia zoezi la kupiga kura. Rais Kais Saied amebadilisha kwa kiasi kikubwa siasa za Tunisia kwa niaba yake tangu katikati ya mwaka 2021 ambapo amejipa karibu mamlaka yote. Wakosoaji wanasema hilo ni sawa na utawala wa mtu mmoja na hivyo uchaguzi wa leo kwa kiasi kikubwa ni sawa na kulichagua bunge lisilo na meno.

Vyama vya upinzani vyasusia uchaguzi wa bunge nchini Tunisia
Vyama vya upinzani vyasusia uchaguzi wa bunge nchini TunisiaPicha: Zoubeir Souissi/REUTERS

Sheria hiyo mpya iliyopitishwa na rais Kais Saied  inahusu kupunguza idadi ya wabunge kutoka  217 hadi wabunge 161, ambao sasa watachaguliwa moja kwa moja badala ya orodha inayopendekezwa na vyama vya siasa. Hivyo basi wabunge ambao hawatimizi wajibu wao wanaweza kuondolewa ikiwa asilimia 10 ya wapiga kura wao watawasilisha maombi rasmi ya kuondolewa kwa mbunge.

Wakosoaji wa rais Saied wanamlaumu kwa kuendesha utawala wa kimabavu amabo wanasema unahatarisha mchakato wa demokrasia ingawa wengine wamesema wanaamini hatua ya kufutilia mbali mtindo wa wabunge kupendekezwa na vyama vyao kutasababisha watu binafsi wawe mbele ya vyama vya kisiasa jambo ambalo litaboresha uwajibikaji wa viongozi waliochaguliwa.

Soma Zaidi:Tunisia yatumbukia katika mgogoro wa kikatiba

Wadadisi wanasema mageuzi ya sheria ya uchaguzi nchini Tunisia yamewaathiri haswa wanawake. Ni wanawake 127 pekee walio miongoni mwa wagombea 1,055 wanaoshiriki kwenye uchaguzi wa Jumamosi.

Neila Zoghlami, rais wa Chama cha Tunisia cha Wanawake wanaounga mkono Demokrasia, amesema sheria ya uchaguzi haikidhi matarajio ya wanawake wa Tunisia. Amesema kwa rais Saied kubadili mfumo na kuamua kutumia mfumo wa wagombea binafsi badala ya kutumia orodha za mapendekezo ya vyama hali hiyokwa namna moja inaongeza idadi ya wanaume wagombea, kwa sababu wananchi wengi wa Tunisia bado wanasitasita kuwapigia kura wanawake.

Rais wa Tunisia Kais Saied
Rais wa Tunisia Kais SaiedPicha: Jdidi Wassim/SOPA/ZUMA/picture alliance

Sghaier Zakraoui, profesa wa maswala ya sheria anayeheshimika alikuwa mmoja kati ya watu wa kwanza waliojitokeza kuunga mkono hatua ya rais Kais Saied ya kujilimbikizia madaraka katika mikono yake lakini kwa zaidi ya mwaka sasa amebadili mawazo. Zakraoui amefafanua kwa kusema kura ya Jumamosi ni sehemu ya matukio binafsi ya rais Kais Saied. Ameeleza kwamba kutokana na rais Saied kuweka katiba na sheria ya uchaguzi kwa ajili yake ni jambo ambalo halitamletea mafanikio yoyote.

Vyanzo:AP/RTRE