1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaKenya

Watu watatu wafa kufuatia mlipuko wa gesi jijini Nairobi

Sylvia Mwehozi
2 Februari 2024

Takriban watu watatu wamekufa na wengine zaidi ya 200 wamejeruhiwa baada ya lori lililokuwa limepakia mitungi ya gesi kuripuka kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

https://p.dw.com/p/4bxOF
Kikosi cha wazima moto kikikabiliana na moto katika eneo bunge la Embakasi
Kikosi cha wazima moto kikikabiliana na moto katika eneo bunge la EmbakasiPicha: Luis Tato/AFP

Msemaji wa serikali Isaac Maigua Mwaura amesema mlipuko huo umesababisha moto mkubwa ambao ulisambaa sehemu kubwa. Mwaura ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kuwa moto huo umeharibu magari kadhaa na mali za biashara, ikiwemo vibanda vya biashara na maduka.

Amesema nyumba za makaazi zilizoko katika eneo jirani pia zimeteketea kwa moto. Mlipuko huo ulitokea usiku wa kuamkia leo kwenye eneo la Embakasi kusini mashariki mwa Nairobi.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesema zoezi la kutafuta manusura bado linaendelea.

"Bado tunatafuta iwapo kuna miili ambayo imeteketea katika nyumba tofauti na tunawaomba Wakenya kutuombea. Huu ni wakati ambao tunahuzunishwa na tukio kama hili ambalo halijawahi kutokea kabla."

Watu 222 waliojeruhiwa walikimbizwa kwenye hospitali mbalimbali. Awali, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema kuwa takribani watu 300 wamejeruhiwa.