1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wasiopungua kumi wauawa katika maandamano mjini Goma

Mitima dela Chance30 Agosti 2023

Watu zaidi ya kumi akiwemo afisa mmoja wa polisi wameuawa kufuatia maandamano ya watu wanaojiita kuwa wa dini ya kizalendo wanaotaka kuikomboa Kongo.

https://p.dw.com/p/4Vk2k
Raia wamekuwa wakiandamana kudai kuondoka kwa wanajeshi wa Monusco
Raia wamekuwa wakiandamana kudai kuondoka kwa wanajeshi wa Monusco Picha: Benjamin Kasembe/DW

Mashuhuda mbalimbali wanasema machafuko hayo yalianza tangu saa kumi asubuhi, haswa katika eneo la Nyiragongo pale kikundi cha vijana wanaojiita Wazalendo wakiwa waumini wa dini inayojidai kuwa ya "Imani ya asili ya Kimasihi na ya Kiyahudi kwa Mataifa” walipojaribu kukaribia kituo cha askari wa ulinzi wa amani wa umoja wa mataifa kwa kifupi MONUSCO mjini Goma kabla ya mapambazuko.

Vijana hao waliovalia kamba, bendera ya dini lao na vitu vingine vya kijadi walikabiliwa na vikosi vya usalama mapema asubuhi.

Kanisa hilo linalojiita la wazalendo linaongozwa na Ephraim Bisimwa, ambaye ndiye mchungaji anayeipinga historia ya Yesu na agano jipya akidai pia kutetea uhuru wa Kongo, wa Afrika na kutaka MONUSCO iondoke bila shaka. Kanisa hili limechomwa moto na Radio ya kanisa hili inayoitwa Uwezo Wa Neno imebomolewa. Katika ujumbe wake alipoitisha maandamano kumepita wiki mbili, Ephraim Bisimwa amesema anajaribu kutetea ujenzi upya wa umoja wa Afrika.

''Wamefunzwa vibaya''

Maeneo kadhaa ya mashariki mwa Kongo yanakaliwa na makundi ya wapiganaji likiwemo lile la M23
Maeneo kadhaa ya mashariki mwa Kongo yanakaliwa na makundi ya wapiganaji likiwemo lile la M23Picha: Michael Lunanga/AFP

Tukio hili limezorotesha shughuli zote katika baadhi ya maeneo ya mji wa Goma na viunga vyake haswa eneo la Ndosho, askari wa Congo na polisi wakiwa wanazunguka huku na kule barabarani ili kurejesha usalama. Tayari waumini zaidi ya thelathini wa dini hii wamekamatwa, kama anavyothibitisha Luteni Kanali Ndjike Kaiko Guillaume, msemaji wa serikali ya kijeshi ya Kivu Kaskazini.

"Tuna mchokozi anayetishia usalama wa Jamhuri na watu hawa wanacheza mchezo wa adui. Wamefunzwa vibaya, wamepewa dawa za kulevya, wamenunuliwa kwa pesa ili kuzidisha ukosefu wa usalama, lakini vyombo vya ulinzi na usalama vimefanya kazi kwa weledi mkubwa." alisema Ndjike. 

Pamoja na kulaani hali ya ukosefu wa usalama Kivu kaskazini, asasi za kiraia mjini Goma zinapinga kwamba hazijakubaliana na mwandalizi wa maandamano hayo zikihofia kwamba huenda idadi ya waliopoteza maisha ni zaidi ya arobaini, watu walioshuhudia wakisema wameona baadhi ya miili ikiwa inasombwa ndani ya magari ya kijeshi Goma.