1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Watu milioni 1.5 wakosa umeme huko Odessa, Ukraine

11 Desemba 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema zaidi ya watu milioni 1.5 kwenye mji wa kusini wa Odessa wamekosa umeme jana Jumamosi baada ya Urusi kufanya mashambulizi ya usiku kucha kwa kutumia ndege zisizo na rubani.

https://p.dw.com/p/4Kmpc
Ukraine-Krieg - Odessa
Picha: Ukrinform/dpa/picture alliance

Kiongozi huyo amesema hujuma zilizofanywa na Moscow kwa kutumia ndege zisizo na rubani ambazo zinashukiwa kuwa zimeundwa nchini Iran, zimeutumbukiza mji wa Odesa na vijiji vingine jirani kwenye giza.

"Hadi sasa, zaidi ya watu milioni 1.5 wa mkoa wa Odessa hawana umeme" amesema hayo Zelenskyy kama alivyokaririwa na shirika la habari la afp.

Hata hivyo serikali ya Ukraine imesema huduma ya umeme bado inapatikana kwenye maeneo muhimu ikiwemo hospitali na wodi za wanawake wajawazito. Hayo yamesemwa na naibu mkuu wa ofisi ya rais wa Ukraine   Kyrylo Tymoshenko aliyesisitiza lakini kuwa "Hali bado ni mbaya, lakini inedhibitiwa".

Mamlaka za mji wa Odessa zimetahadharisha kwamba matengenezo ya miundombinu iliyoharibiwa yanaweza kuchukua muda wa kati ya wiki kadhaa au hadi miezi mitatu.

Mji huo ulio kwenye mwambao wa Bahari Nyeusi ulikuwa kitovu cha shughuli za watalii wengi kutoka Urusi na Ukraine kabla ya rais Vladimir Putin kutuma vikosi vyake nchini Ukraine mnamo Februari 24.

Ndege za "kamikaze" zashambulia usiku kucha mkoani Odessa 

Ukraine-Krieg - Odessa
Watembea kwa miguu wanalazimika kupita kwenye mji ulio na giza totoroPicha: Ukrinform/dpa/picture alliance

Gavana wa mkoa wa Odessa, Maksym Marchenko, amesema droni za Urusi zinazofahamika kama "kamikaze" zilifanya hujuma usiku kucha wa kuamkia siku ya Jumamosi.

Mashambulizi hayo yamefanya wilaya zote za mkoa huo kukosa umeme. Vikosi vya Ukraine vilifanikiwa kundugua ndege mbili zisizo na rubani.

Mnamo siku ya Ijumaa, Ukraine ilisema majimbo ya kusini mwa nchi hiyo ndiyo yanapitia kipindi kigumu cha kukosekana kwa umeme baada ya mfululizo wa mashambulizi ya Urusi yanayoilenga gridi ya taifa.

Urusi ilifyetua makombora kadhaa yaliyoipiga miundombinu ya gridi ya umeme ya taifa nchini Ukraine na kuongeza shinikizo kubwa kwa nchi ambayo tayari inataabika na mifumo ya umeme iliyoharibiwa.

Urusi yasema miundombinu ya umeme itaendelea kulengwa 

Urusi ilianza kuilenga miundombinu ya umeme nchini Ukraine, baada ya kupoteza maenep kadhaa kwenye uwanja wa vita na vikosi vya Kyiv kusonga mbele.

Ukraine Odessa | Russische Panzer mit Graffiti
Picha: Instagram/@lbws_168

Mnamo Alhamisi iliyopita, rais Vladimir Putin wa Urusi alisema ataendelea kuihujumu gridi ya taifa ya Ukraine licha ya miito ya kutaka vikosi vyake vikomeshe mashambulizi yanayoilenga miundombu ya kiraia.

Hujuma hizo zimepelekea mgao mkbwa wa umeme nchini Ukrainemkatika kipindi cha sasa cha baridi kali.