1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu mil 114 wakimbia makazi yao kutokana na vita duniani

Hawa Bihoga
31 Mei 2024

Idadi ya watu wanaokimbia makaazi yao kutokana na kuongezeka kwa vita, ghasia na mateso imeongezeka ulimwenguni na kufikia watu milioni 114. Baraza la Usalama a UN limeshutumiwa kwa kushindwa kuchukua hatua.

https://p.dw.com/p/4gUQO
New York | UN-Hochkommissariat für Flüchtlinge | Filippo Grandi
Picha: Lev Radin/Pacific Press Agency/IMAGO

Hayo yamesemwa na mkuu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, , ambaye amelikosoa vikali Baraza la Usalama la Umoja huo kutokana na kile alichosema ni kushindwa kukabiliana na mizozo hiyo.

Katika hotuba yake mbele ya Baraza la Usalama hapo jana Alhamisi, Grandi alitumia maneno makali akisema baraza hilo, ambalo ni chombo cha juu katika Umoja huo, limeshindwa kutumia madaraka yake katika kutataua migogoro ambayo inaendelea katika maeneo mbalimbali ulimwenguni akianzia vita vya Gaza, Ukraine, Sudan, Myanmar hadi eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na maeneo mengine ulimwenguni.

Aidha aliyashutumu baadhi ya mataifa ambayo hakuyataja moja kwa moja kwa majina kwa kufanya maamuzi ya "sera za kigeni zenye maono fupi", ambayo mara nyingi yana msingi wa undumilakuwili, ukiukwaji wa sheria na kutotumia nafasi yao katika baraza hilo la usalama ili kulinda amani na usalama.

Soma pia:UNHCR: Wakazi wa Gaza hawapaswi kuvuka kuingia Misri

Akizungumzia ukiukwaji wa sheria za kimataifa katika ulinzi wa haki za binaadamu, Grandi amesema kutofuatwa kwa sheria hizo kumesababisha kuongezeka kwa mizozo kila pahala ulimwenguni, idadi ya vifo vya raia, huku  unyanyasaji wa kijinsia ukitumika kama silaha kwenye vita, na miundombinu ya kiraia ikiwemo shule na hospitali ikishambuliwa na kuharibiwa vibaya, na wafanyakazi wa mashirika ya kiutu wanaotoa misaada kwenye mizozo wakigeuka kuwa walengwa kwenye mapigano.

"Tumechelewa mno kwani tayari makumi kwa maelfu ya watu wameshauawa huko Gaza, Ukraine, Kongo, Myanmar na maeneo mengine mengi."

Aliliambia Baraza la Usalama akiongeza kwamba "lakini hatujachelewa kuwa makini na kuchukuwa hatua kwenye migogogoro ambayo bado haijatatuliwa, ili isiongezeke na kuripuka kwa mara nyingine."

"Bado hatujachelewa kuongeza msaada kwa mamilioni ya watu ambao wamehamishwa kwa nguvu kurejea nyumbani kwa hiari, kwa usalama na heshima. Bado hatujachelewa kujaribu kuwaokoa mamilioni zaidi kutoka kwenye janga la vita." Alisema huku akiweka msisitizo kuwa kuna haja ya kuchukua hatua muhimu za bila kujali maslahi kati ya taifa na taifa.

Kwanini Baraza la Usalama linashindwa kumaliza mzozo?

kutofikia muafaka wa kukabiliana na mzozo ulimwenguni, Grandi amelinyooshea kidole Baraza la Usalama kutokana na kuzidi kuwa na mgawanyiko, na wanachama wake watano wa kudumu wenye kura ya turufu kuzidi kutofautiana, huku Marekani, Ungireza na Ufaransa mara nyingi zikipinga hoja za Urusi na China.

Israel epusheni mauaji ya halaiki Gaza

Kauli ya Grandi inafuatia ukweli kwamba chombo hicho cha juu cha Umoja wa Mataifa hakijafikia maamuzi yoyote kuhusu vita katika eneo la Ukanda wa Gaza, ikiwemo kutoa wito wa usitishwaji wa mapigano kutokana na upinzani uliopo kutoka kwa Marekani na mshirika wake wa karibu Israel.

Soma pia:Baraza la Usalama la UN halijaafikiana juu ya Palestina

Kwa upande wa mzozo wa Ukraine, Baraza hilo halijafiakia suluhu kwani Urusi ambae ni muhusika mkuu katika vita hivyo vilivyodumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa, angelitumia kura yake ya turufu kuzuia azimio lolote juu ya vita hivyo vilivyogharimu maisha ya maelfu ya watu na kuharibu vibaya miundombinu ya kiraia.